December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mwanafunzi wa kidato cha kwanza afariki baada ya kuangukiwa na jiwe,akitekeleza adhabu

Judith Ferdinand, Timesmajira online Mwanza

Mwanafunzi mmoja wa shule ya sekondari Mwinuko Kata ya Kitangiri Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza amepoteza maisha baada ya kuangukiwa na jiwe huku mmoja akipata majeraha ya kuvunjika mguu wa kulia.

Akizungumzia tukio hilo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, SACP.Wilbroad Mutafungwa ameeleza kuwa tukio hilo limetokea Machi 17,2023 majira ya saa moja asubuhi katika eneo la shule ya Sekondari Mwinuko.

Ambapo wanafunzi walikuwawanatekeleza adhabu waliyopewa na Mkuu wa Shule hiyo baada ya kukamatwa wanaongea lugha ya Kiswahili kinyume na taratibu za shulehiyo ambayo wanatakiwa kuzungumza lugha ya kingereza wawapo shuleni.

Baada ya kupewa adhabu hiyo iliyotolewa jana Machi 16,2023 na Mkuuwa Shule hiyo, baadhi ya wanafunzi walitekeleza adhabu hiyo ambapo waliambiwa kuchimba kifusi na kujaza sehemu zenye mabonde, lakini Glory Faustine na Emmanuel Michael hawakukamilisha adhabu hiyo.

“Ilipofika asubuhi ya leo walifika shuleni hapo kwa ajili ya kukamilisha adhabu,wakiwa ndani ya shimo lenye kifusi ghafla waliangukiwa na jiwe kubwa lililokuwa juu ya shimo hilo na kusababisha kifo kwa mwanafunzi aitwayeGlory Faustine,mwenye umri wa miaka 14, mwanafunzi wa Kidato chaKwanza,Mkazi wa Kirumba,”.

Huku jiwe hilo likisababisha majeraha kwa Emmanuel Michael, mwenye umri wa miaka 13, mwanafunzi wa kidato cha kwanza, mkazi wa Ibanda Busisi ambaye amevunjika mguu wa kulia.

Mutafungwa ameeleza kuwa kufuatia tukio Hilo Jeshi la Polisi linamshikilia Mwalimu Mkuu wa shule ya Secondari Mwinuko aitwaye Mwalu Steven mwenye umri wa miaka 51, mkazi waBuhongwa pamoja na mwalimu aliyekuwa zamu siku hiyo aitwaye Theonest Malosha, mwenye umri wa miaka 35,mkazi wa Kahama Buswelukwa mahojiano zaidi.

Pia ameeleza kuwa mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Sekou-Toure na utakabidhiwa kwa ndugu baada ya uchunguzi nahali ya majeruhi inaendelea vizuri.

Hata hivyo Jeshi hilo linatoa rai kwa wananchi na wazazi kuendelea kuwa nasubra katika kipindi hiki ambacho linafanya kila namna kuhakikisha linachukua hatua za kisheria kwa yeyote aliyehusika aidha kwa uzembe aukwa kutotimiza wajibu wake ipasavyo.