November 14, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mwanafunzi  atengeneza roboti utambuzi wa vifaa vya milipuko

Na Penina Malundo,timesmajira, Online

MWANAFUNZI wa Mamlaka ya Elimu na Ufundi Stadi (VETA) Kigoma, Innocent Simon ametengeneza roboti (military security Robort) kwa ajili kusaidia kutambua vilipuzi na mahali ilipotegwa vifaa vya milipuko katika masuala ya ulinzi kwenye jamii na kwenye maeneo ya matukio yenye hatari ya vita au uvunjifu wa amani. 

Akizungumza leo na waandishi wa habari  kwenye banda la VETA katika Maonesho ya 46 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam(DITF), Simon amesema roboti hiyo

 inaweza kufanya kazi hiyo kwa kutumia rimoti ya betri au umeme kwa kusimamiwa na mtu ambaye huiendesha bila kuwa eneo la tukio kwa umbali wowote ule. 

“Kwa mfano kama kuna mahali kumetegwa mabomu au vilipuzi vyovyote, roboti hii ina uwezo wa kutoa taarifa kwa kutoa ishara ya sauti na kuonyesha mahali kilipuzi kilipo kwa sababu kimefungwa kamera,” amesema na kuongeza 

“Kazi ya doria ya ulinzi inayofanywa na jeshi la polisi usiku, hii roboti inaweza kusaidia katika hilo, kwa hiyo hata kama askari wanakwenda inakuwa rahisi wanakuwa na muongozo,”alisema Simon

Amesema kazi nyingine ni kusaidia kutambua mahali vilipofichwa vilipuzi au milipuko na kurahisisha kazi kwa majeshi au walinda usalama kukabiliana na adui kwa urahisi hususani katika maeneo ya vita au mahala panapopangwa kufanyika uhalifu.

Simon amesema sehemu nyingine ambapo roboti hiyo inaweza kufanya kazi ni pamoja na kwenye maeneo ya Bandari na Viwanja vya ndege.

“Mfano kwenye viwanja vya ndege, inaweza kutumika kusaidia katika suala la ukaguzi kwa ajili ya kubaini wale wahalifu wanaojaribu kupita na dawa za kulevya au bidhaa yoyote haramu,” amesema Simon