November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mwanafunzi afariki kwa kupigwa shoti ya umeme

Na Fresha Kinasa, Mara

MWANAFUNZI Kevin Magiri (14) anayesoma katika Shule ya Msingi Murunyigo mkazi wa Kijiji cha Kihemba katika Halmashauri ya Wilaya ya Musoma mkoani Mara, amefariki dunia baada ya kunaswa na nyaya za umeme wakati akiwa amepanda juu ya mti ulio kwenye njia ya umeme.

Akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na tukio hilo mwishoni mwa wiki, Kaimu Meneja wa TANESCO Mkoa wa Mara Mhandisi Meshack Laurent alisema, mwanafunzi huyo alifariki dunia Aprili 2, mwaka huu katika Kitongoji cha Kihemba baada ya kunaswa na nyaya akiwa juu ya mti aliokuwa amepanda na baadaye kuanguka chini kabla ya kupatwa na umauti.

“Tulipokea taarifa siku ya tukio majira ya saa nane mchana kupitia kitengo chetu cha dharura ambapo Juma Magesa alieleza kuna mtoto kanaswa na umeme maeneo ya Kijiji cha Kihemba, ambapo mtu wa dharura pia akazileta taarifa hizo kwangu Kaimu Meneja,nililazimika kuomba msaada wa usalama Polisi Mkoa wa Mara, lakini waliniambia kule tayari kuna polisi watakuwepo,”alisema.

“Niliambatana na Afisa Mahusiano na Afisa Usalama wa TANESCO na kundi la dharura tulifika na kukuta kweli mtoto wa miaka 14 kafariki. Mazingira ya tukio ni kwamba alipanda juu ya mti uliokuwa karibu na njia ya umeme ndipo akapigwa shoti akaanguka kutoka mtini, lakini mashuhuda walisema alipoanguka chini alikuwa akipumua ndipo baadaye akakata roho,”alisema.

Aidha alielezea changamoto ambayo wamekuwa wakikumbana nayo wakati wa kukata miti inayokaribiana na njia za umeme kuwa, ni pamoja na baadhi ya wananchi kutokuwa tayari kuruhusu miti yao ikatwe licha ya kwamba, miti hiyo ambayo ipo karibu ma njia za umeme ni hatari kwa usalama na hivyo akaitaka jamii kutoa ushirikiano ili kuepisha matukio ambayo yanaweza kujitokeza isipokatwa.

Kwa upande wake Afisa Mahusiano na Huduma kwa Wateja wa TANESCO Mkoa wa Mara, James Vesso alisema, wamekuwa wakitoa elimu kwa jamii na shule za msingi na sekondari kwa kushirikiana na EWURA juu ya kulinda miundombinu ya shirika hilo.

Sambamba na matumizi bora ya umeme na usalama, huku pia akifafanua kuwa wananchi watoe ushirikiano kwa TANESCO wanapotaka kukata miti iliyokaribu na njia za umeme ili iweze kukatwa bure kwa hali ya usalama na shirika hilo.

Pia,aliwaasa wananchi wanaotayarisha mashamba kwa ajili ya shughuli za kilimo wahakikishe wanalinda na kutunza miundombinu ya TANESCO kwani ikilindwa itadumu kwa muda mrefu na kuchangia kuliletea mapato shirika hilo na kutoleta madhara yoyote yale kwa wananchi katika maeneo yote mkoani hapa.

Aidha Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Daniel Shillah, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo.