Na Joyce Kasiki,Dodoma
MBUNGE wa Mbeya Mjini, Patrick Mwalunenge, ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa hatua kubwa zilizopigwa katika utekelezaji wa Mkakati wa Nishati Safi ya Kupikia, akisema ajenda hiyo imeleta matokeo chanya kwa wananchi, hususan wanawake na jamii za vijijini.
Akichangia mjadala wa Mipango ya Utekelezaji wa Dira ya Taifa ya 2050 bungeni jijini Dodoma, Mwalunenge alisema matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini yameongezeka kwa kasi, kutoka asilimia 6.9 hadi 23.2, hatua aliyoitaja kuwa mafanikio makubwa ya kisera na kiuongozi.
Mbunge huyo alieleza kuwa wanawake, wakiwemo wa Mkoa wa Mbeya ambao walimpa kura za kumwakilisha bungeni, ni miongoni mwa wanufaika wakubwa wa mpango huo, hasa kutokana na mzigo wa kazi za kupikia na athari za kiafya zinazotokana na matumizi ya nishati zisizo safi.
Katika mchango wake, Mwalunenge alimpongeza Rais Samia kwa kutoa ruzuku ya asilimia 50 kwa mitungi ya gesi ya kilo sita 452,445, pamoja na ruzuku ya asilimia 85 kwa usambazaji wa majiko banifu 200,000, yaliyolenga wananchi waishio vijijini.
“Nishati safi ni uchumi, nishati safi ni afya, na nishati safi ni mazingira,” alisema Mwalunenge, akisisitiza umuhimu wa kuendelea kupanua wigo wa elimu ya matumizi ya nishati safi kwa wananchi, kama ilivyoelekezwa kwenye mkakati wa nishati safi ya kupikia uliozinduliwa na Rais mwezi Mei 2024.
Aidha, aliishauri Serikali kuongeza upatikanaji wa majiko ya gesi na majiko banifu yenye ruzuku, huku akizipongeza taasisi 1,136 ambazo tayari zimeitikia wito wa kutumia nishati safi ya kupikia kwa vitendo.
Hata hivyo, alisema bado zipo taasisi ambazo hazijaunga mkono juhudi hizo, na kushauri kuwepo kwa sheria, kanuni na miongozo itakayozilazimisha taasisi zote zinazohudumia watu zaidi ya 100 kutumia nishati safi ya kupikia.
“Isiwe tena hiari, iwe ni lazima kwa mujibu wa sheria, ili tulinde mazingira yetu,” alisisitiza.
Mwalunenge pia alibainisha kuwa kwa sasa kaya zipatazo 2,000 zinatumia gesi asilia kwa ajili ya kupikia, na kushauri kuongezwa kwa wigo wa matumizi ya gesi hiyo majumbani. Vilevile, alisisitiza umuhimu wa kuvutia uwekezaji zaidi katika sekta ya nishati safi ya kupikia.
Katika mapendekezo yake, Mbunge huyo aliishauri Serikali kupunguza tozo na kodi kwenye nishati safi, teknolojia zake pamoja na mashine za kutengeneza majiko, ili kupunguza gharama kwa wananchi. Pia alipendekeza kuanzishwa kwa mifumo ya “lipa kadri unavyotumia” (pay as you use) kwa gesi, ili kuongeza uwezo wa wananchi wengi kuimudu.
Mwalunenge alisema mafanikio yaliyopatikana chini ya uongozi wa Rais Samia yanapaswa kuungwa mkono kwa kuweka mazingira bora zaidi ya uwekezaji, ili sekta ya nishati safi ya kupikia iendelee kukua na kuwanufaisha Wananchi.

More Stories
Kihongosi amtaka mkandarasi kuwalipa vibarua stahiki zao
DC Mbozi afuturisha wananchi, asisitiza mshikamano na Umoja.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali: Nina imani mubna utendaji kazi wa ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria