January 17, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mwalimu Mkuu Sinza amualika Waziri Ummy shuleni kwake

Na David John,Timesmajira Online.

MWALIMU Mkuu wa Shule ya Msingi Sinza iliyopo Manispaa ya Ubungo mkoani Dar es Salaam, Elizabeth Joseph amemuomba Waziri wa Nchi, ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TMISEMI), Ummy Mwalimu kufika shuleni hapo ili kujionea shule hiyo ilivyochakaa, licha ya juhudi mbalimbali zinazofanywa na kuona namna ya kuiboresha.

Amesema shule hiyo ambayo imejengwa tangu 1976, miundombinu yake imechakaa na hata Ofisi ya Mwalimu Mkuu hakuna pamoja na kwamba shule hiyo, imekuwa ikifanya vizuri katika matokeo yake ya darasa la saba na kwa miaka mitatu mfululizo, wamekuwa ndani ya 20 bora kitaifa na kushika na fasi ya saba.

Elizabeth ametoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam kwenye sherehe za Sikukuu ya Wafanyakazi (Mei Mosi ), ambapo katika mkoa wa Dar es Salaam zilifanyika kwenye Uwanja vya Uhuru ambapo mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Mkoa, Abubakar Kunenge ambapo mwalimu huyo alitunukiwa tuzo ya mfanyakazi bora.

“Nasikia furaha sana na kwa kwa kweli, tuzo hii imeniheshimisha mno licha ya miundombinu chakavu iliyopo shuleni kwangu na kukosa Ofisi ya Mwalimu Mkuu, bado tumeweza kufanya vizuri kwenye matokeo ya darasani na hatimaye mimi kama Mwalimu Mkuu wa shule tangu 2016/12 nimepata tuzo hii,” amesema.

Pia amewapa ujumbe walimu wake kuwa ualimu ni wito, hivyo waendelee kufanya kazi kwa kujituma zaidi na kwa umoja na kushirikiana, ili kuendelea kukuza elimu nchini.

Akizungumzia hotuba ya mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa, Mwalimu Elizabeth amesema wao kama wafanyakazi wamefarijika kwa maneno mazuri ya bosi huyo wa mkoa kwani ameyachukua mapendekezo yao na maoni yao, hivyo yapo ambayo yatafanyiwa kazi kama mkoa na yale ya kitaifa ni ya kisera.

Amesema Mkuu wa Mkoa, ametupa moyo na amesema ifikapo Mei Mosi ya mwakani atakuja kueleza yale ambayo kwa upande wake, atakakuwa ameyashughulikia hivyo wao kama walimu wanamshukuru.

Wakati huo huo, Mwalimu Shaban Mussa ambaye anafundisha somo la kingereza shuleni hapo naye amepokea tuzo ya Mwalimu Bora wa darasa, huku akimshukuru Mwalimu Mkuu wake kwa kumuunga mkono katika safari yake ya ualimu.

Amesema tuzo hiyo, imemfanya aongeze juhudi zaidi lakini ameingia kwenye vitabu vya walimu bora hivyo anamshukuru Mungu, pamoja na Chama cha Wafanyakazi kwa kumuona kuwa na yeye ni bora.