October 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mwakinyo atamba kumpiga TKO Muargentina

Na Mwandishi wetu, TimesMajira online

BONDIA wa Kimataifa wa Tanzania, Hassan Mwakinyo ametamba kuandika historia nyingine kubwa katika mchezo wa ngumi kwa kumtwanga kwa ‘Technical Knock out (TKO)’ mpinzania wake Jose Carlos Paz raia wa Argentina.

Mwakinyo na Paz watapambana ulingoni Ijumaa ya Novemba 13 katika pambano la raundi 12 la kuwania ubingwa wa Mabara uzito wa Super Welter unaotambuliwa na chama cha WBF litakalofanyika kwenye ukumbi wa Next Door Arena.

Pambano hilo litashuhudiwa na rais wa Chama cha Ngumi za Kulipwa cha WBF, Howard Goldberg ambaye anatarajiwa kuwasili hapa nchini leo Novemba 11 kwa ajili ya kusimamia pambano hilo.

Goldberg ambaye anakuja hapa nchini kwa mara ya sita kwa ajili ya kusimamia ngumi za kulipwa, atawasili pamoja na mwamuzi wa pambano hilo Edward John Marshall.

Akizungumza Dar es Salaam, Mwakinyo amesema kuwa, atahakikisha mpinzani wake Paz anaachana na mchezo wa ngumi za kulipwa kutokanana kipigo alichumuandalia.

“Natamani pambano lifanyike mapema iwezekanavyo, hata siku moja kabla kwani nipo fiti zaidi ya nilivyokuwa mwanzoni. Sitaki kuwanyong’onyesha Watanzania katika pambano hilo,” amesema Mwakinyo.

Amesema, anajua kuwa Paz ni bondia mzuri na amejiandaa vyema katika pambano hilo, lakini kutokana na jinsi alivyoandaliwa na kambi yake, hatokuwa na nafasi ya kutamba kwake.

Licha ya tambo hizo za Mwakinyo, mpinzani wake Paz amesema kuwa, hakuja nchini kutembea zaidi ya kuwania ubingwa huo anaoushikilia Mwakinyo hivyo ni lazima aondoke nao.

“Nipo vizuri, mazoezi yangu nchini yamekuwa na mafanikio makubwa na hali ya hewa siyo tatizo hivyo nitahakikisha nakwenda kumfundisha ngumi Mwakinyo ,” amesema Paz.

Pambano hilo litasindikizwa na mapambano ya utangulizi yatakayowakutanisha bondia Hussein Itaba dhidi ya mpinzani wake kutoka DR Congo, Alex Kabangu, Fatuma Zarika atazichapa na Patience Mastara kutoka Zimbabwe wakati Mtanzania Zulfa Macho atazichapa na Alice Mbewe wa Zambia ambapo kila mmoja ametamba kumgalagaza mpinzani wake.

Kuelekea katika pambano hilo, Mkurugenzi wa Jackson Group Sports, Kelvin Twissa amesema, hadi sasa maandalizi yote yameshakamilika na kuwaomba mashabiki kuendelea kununua tiketi kwa ajili ya kushuhudia burudani safi katika pambano hilo.

“Maandalizi yapo vizuri na kama mnavyoona mabondia wote wapo hapa na sas tunamsubiri Rais wa EBF, Howard Goldberg na mwamuzi Edward John Marshall ambao watawasili leo Jumatano Novemba 11,” amesema Twisa.