July 8, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mwakilema aitaka Korogwe TC kukusanya kodi kwa ‘control number’

Na Yusuph Mussa, Timesmajira Online,Korogwe

MKUU wa Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga William Mwakilema ameitaka Halmashauri ya Mji Korogwe kukusanya kodi ya pango la vibanda vya wafanyabiashara soko la Manundu kwa kutumia Kumbukumbu ya malipo (Control Number) badala ya POS mashine.

Kwani ana uzoefu wa baadhi ya halmashauri nchini kumegundulika mashine hizo za kukusanya fedha kwa njia ya kielektroniki ni miradi ya watu binafsi lakini fedha ikikusanywa kupitia Control Number inakwenda moja kwa moja serikalini.

Mkuu wa Wilaya ya Korogwe William Mwakilema akizungumza kwenye mkutano wa wafanyabiashara Korogwe

Pia ameitaka halmashauri hiyo kulipa madeni kwa wazabuni walioshiriki kujenga miradi ya Serikali kwa kununua vifaa vya ujenzi kupitia miradi iliyojengwa kwa Force Account huku akiwataka waliotoa vifaa hivyo vya ujenzi wapeleke vielelezo ofisini kwake vinavyoonesha wamefanya kazi na hawajalipwa fedha zao wengine tangu awamu ya tano.

Mwakilema ameyasema hayo Juni 3, 2024 kwenye mkutano ulioitishwa na Jumuiya ya Wafanyabiashara Korogwe, na kumualika Mkuu wa Wilaya kusikiliza kero zao ambayo moja wapo ni wafanyabiashara kufanya kazi na halmashauri lakini hawalipwi fedha zao.

“Nina uzoefu hasa ule uliotokea Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya, baadhi ya watumishi wasio waaminifu wanafanya POS kama miradi yao lakini ukikusanya fedha kwa Control Number ina uhakika wa kwenda serikalini moja kwa moja na ikitokea kukusanya kwa POS iwe kwa mazingira magumu,jambo hili mlishakubaliana na wafanyabiashara, iweje mkusanye kwa Control Number kwa mwezi mmoja halafu mrudi tena kwenye POS Mashine,”amehoji Mwakilema na kuongeza kuwa;

“Pia nataka halmashauri kuwalipa fedha zao wafanyabiashara wote waliofanya kazi za ujenzi wa miundombinu,wanapofanya kazi ni lazima walipwe hawa watu wana mambo mengi, wanatakiwa kuhudumia familia zao, kupeleka mapato TRA na kulipa mikopo, hivyo muwalipe fedha zao, na nataka Marandu uje na vielelezo vyote vinavyoonesha umefanya kazi na halmashauri,”.

Mfanyabiashara Edistariki Marandu akitoa malalamiko yake kwa Mkuu wa Wilaya ya Korogwe William Mwakilema

Wakitoa malalamiko yao, mfanyabiashara wa soko la Manundu Abdallah Shemmea amesema kila mwezi analipa sh. 30,000 ya pango kwa Halmashauri ya Mji Korogwe huku mwezi mmoja tu ndiyo wamelipa kwa kutumia Control Number lakini miezi mingine wanaletewa POS Mashine.

Mfanyabiashara Edistariki Marandu amesema anaidai Halmashauri ya Mji Korogwe milioni 36.2 baada ya kupeleka vifaa kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya Serikali pamoja na vifaa vya ukarabati wa umeme.

Baadhi ya sehemu alikopeleka vifaa hivyo ni shule ya msingi Mbeza anadai milioni moja,shule ya msingi Mgombezi 550,000, shule ya sekondari Chifu Kimweri milioni tano,shule ya sekondari Old Korogwe milioni 2.9,zahanati ya Kwamsisi milioni 6.8,shule ya msingi Kwasemangube milioni 2.9, Hospitali ya Magunga jengo la meno milioni 1.7 na shule ya msingi Kitopeni (madarasa ya Boost) milioni 3.6.

“Mkuu, nimekwenda mara kadhaa kudai fesha zangu kwa Mhasibu (Mweka Hazina) wa halmashauri, lakini ananieleza hajui madeni hayo,” amesema Marandu.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Korogwe Francis Komba akijibu baadhi ya hoja za wafanyabiashara



Mfanyabiashara Alphonce Kimario amesema moja ya changamoto wanayoipata kushindwa kulipwa fedha zao baada ya wao kukopesha vifaa ni walimu kushindwa kueleza ukweli wa maeneo wanayojenga vyumba vya madarasa na miundombinu mingine.

“Walimu wanatengeneza madeni kwenye ujenzi wa miundombinu,wanashindwa kusema ukweli kutokana na sababu za kisiasa.Mfano Mwalimu wa shule ya Msingi Mbeza anapoelezwa ajenge darasa kwa milioni 20 anaweza kumaliza ujenzi wake, lakini Mwalimu wa shule ya msingi Kwamkole, hawezi kujenga darasa kwa milioni 20 likakamilka hiyo ni kutokana na eneo hilo kuwa na mlima hivyo kutumia gharama ya ziada,” na kuongeza kuwa;

“Matokeo yake wanaongeza vifaa ili kukamilisha jengo wakati fedha za kuendelea na jengo hilo zimekwisha hivyo kushindwa kulipa wasambazaji wa vifaa vya ujenzi,”.

Wafanyabiashara wakiwa na wageni wengine kwenye mkutano