March 9, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mwakalosi:Watanzania wanaweza kuwa na hali bora zaidi wakitumia kiwango kikubwa cha gesi

Na Penina Malundo,Timesmajira

Afisa Mkuu wa Uhusiano na Mawasiliano, kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Wilfred Mwakalosi amesema watanzania wanaweza kuwa na hali bora zaidi kama watatumia kiwango kikubwa zaidi cha gesi asilia kwenye usafiri na usafirishaji hali itakayosaidia gharama za usafiri kupungua.

Ameyasema hayo leo wakati akiwasilisha mada kwenye Kongamano na maonesho ya Petroli ya Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAPCE’25),amesema sekta ya usafiri ndio sekta mama ya mambo yote.”Kwani gharama za usafiri zikiwa kubwa hata kufika Songea gharama zitakuwa kubwa zaidi ,hata mafuta yenyewe kuyasafirisha gharama zake zinakuwa kubwa hivyo tukitumia gesi asilia gharama zitapungua kwa kiasi kikubwa,”amesema Mwakalosi.

Utafiti ulilenga kuchunguza faida gani za kiuchumi na kijamii zitapatikana iwapo kama taifa litaamua kutumia kwa kiwango kikubwa gesi asilia kwenye usafiri na usafirishaji.

Amesema matokeo ya utafiti huo yanaonesha kwamba ni kweli gesi ikitumika hasa katika usafiri wa umma ikiwemo kwa. Malori,Mabasi na tax ni dhahiri kwamba gharama za usafiri zitakuwa chini.

“Hii maana yake faida ya gharama ya kupanda kwa mafuta itadhibitiwa kwa kiasi fulani,hata uchafuzi wa hewa kupitia mafuta itasaidia kupungua kwani ukitumia gesi safi itapunguza uchafuzi wa hali ya hewa,”amesema

Amesema gesi inayopatikana nchini kama itatumika katika usafiri na usafirishaji itkuwa na manufaa makubwa kwa kuzigatia kwamba gharama yake ipo chini.”Lita moja ya mafuta ya Diseli au Petroli inaenda kwa gharama ya sh.2700 au 2800 lakini kilo moja ya Gesi Asilia ni sh. 1550 unaona gharama yake ilivyodogo na watu kutoshindwa kutumia,”amesema.

Aidha katika wasilisho lake ameishauri serikali kutengeneza sera ambazo zitatoa kipaumbele katika matumizi ya gesi asilia,

kwani serikali inamagari mengi kuliko wamiliki wote hivyo ikionesha nia ya dhati kwa kubadilisha magari kutumia gesi asilia itakuwa imeokoa fedha nyingi za mafuta.

“Pia sera ielekeze vyombo vya usafirishaji kutumia nishati ambayo ni nafuu zaidi ili kutoa unafuu katika uwekezaji wa vituo vya CNG kwani hadi sasa kuna vituo vichache nchini ikiwemo Mtwara,Lindi na Dar es Salaam,”amesisitiza.