March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mwaifunga amuombea kura Dkt.Samia

Na Mwandishi Wetu Timesmajira Online-Tabora

WAKAZI wa Mkoa wa Tabora wameombwa kumpigia kura za kishindo mgombea kiti cha Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM),Dkt.Samia Suluhu Hassan,kwa kuwa ana maono ya maendeleo ni na mchapa kazi.

Hayo yameelezwa na mgombea Ubunge Jimbo la Tabora Mjini kupitia CCM,Hawa Mwaifunga,wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa kampeni uliofanyika Kata ya Cheyo, Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.

Amesema kuwa katika kipindi cha miaka 4 ya uongozi wake, Dkt. Samia, amefanya mambo makubwa katika Kata hiyo na Jimbo zima la Tabora Mjini hivyo akaomba wampe mitano tena ili apaishe Mkoa huo kimaendeleo.

Ametaja baadhi ya mambo yaliyofanyika kuwa ni ujenzi wa miundombinu bora ya elimu katika shule za msingi na sekondari ambapo shule zote katika manispaa hiyo sasa hivi zina mazingira bora ya kujifunzia na kufundishia.

Pia huduma za afya zimeboreshwa kwa kiasi kikubwa na kusaidia wakazi wa Jimbo hilo kupata matibabu karibu na maeneo yao hivyo kutotumia gharama kubwa kufuata huduma hizo nje ya Manispaa hiyo.

Aidha mpango wa elimu bure kwa watoto wote kuanzia shule ya awali hadi kidato cha sita umesaidia kuondoa matabaka ya elimu kwa watoto wote nchini hivyo kuwawezesha kupata elimu pasipo kikwazo.

“Dkt.Samia ni kinara wa maendeleo,niwaombe Oktoba 29 mwaka huu tujitokeze kwa wingi kumpigia kura za kishindo,pia na mimi mnipigie ili niwe Mbunge wenu na Yusuph Kitumbo awe Diwani wa kata hii,”amesema.

Kwa upande wake mgombea Udiwani wa Kata ya Cheyo kupitia CCM,Yusuph Kitumbo, amesema katika utekekalezaji wa ilani ya uchaguzi ya chama hicho ya 2020-2025,katika kata hiyo zimejengwa barabara za lami za kutosha na kuboresha vyumba vya madarasa katika shule zote.

‘Ndani ya miaka mitano, kata yetu imekuwa mfano wa kuigwa kimaendeleo katika sekta za elimu, afya na barabara, hata matokeo ya darasa la saba, kata yetu ndiyo inayoongoza kwa Mkoa mzima, nichagueni ili niyasimamie vizuri haya,”ameeleza.