March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

MWADETA yaandaa walimu kuhudumia watoto wenye kichwa kikubwa,mgongo wazi

Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online-Magu

Taasisi ya Mwanangu Development Tanzania (MWADETA) imeendelea kuwa nguzo muhimu kwa watoto wenye changamoto ya kichwa kikubwa na mgongo wazi, baada ya miaka 10 ya kuwasaidia kupata matibabu.

 Hata hivyo, taasisi hiyo imebaini changamoto nyingine  inayowakabili kwa  sasa  watoto hao ni  kukosa fursa ya elimu kutokana na mazingira ya shule kutokuwa rafiki kwao.

Hayo yamebainishwa Novemba 20,2025 na Ofisa Mradi wa Wezesha mtoto kutokana MWADETA unaofadhiliwa na shirika Beyond Inclusive,Peter David,katika mafunzo ya kuwajengea uwezo wa namna ya kuwasaidia watoto wenye  changamoto ya kichwa kikubwa na mgongo wazi kwa walimu 15 kutoka shule za msingi tatu za Serikali kutoka Wilaya ya Magu ikiwemo Kitongosima, Wita na Itumbili ambayo ina Kitengo cha watoto wenye mahitaji maalumu.

Amesema kutokana na  watoto wengi wenye changamoto  hiyo kutoweza kujizuia haja kubwa na ndogo imekuwa kikwazo cha  wao kupata haki ya elimu,kwani inawafanya wakataliwe au kuhofia kwenda shuleni kwa hofu ya kuchekwa na kudhalilishwa pamoja na 

baadhi ya walimu kukosa uelewa wa namna ya kuwahudumia.

Peter amesema,baada ya kubaini changamoto  hiyo MWADETA imeanza kutekeleza mafunzo maalumu kwa walimu ili kuongeza ujuzi na uelewa wa kuhudumia watoto wenye kichwa kikubwa na mgongo wazi kupitia mradi wa Wezesha mtoto.

“Hatua hii inalenga kuhakikisha shule za Serikali zinakuwa salama, jumuishi na zenye uwezo wa kuwapokea watoto hao bila ubaguzi.Kupitia mafunzo hayo, walimu wamefundishwa namna ya kuwasaidia watoto wasioweza kuzuia haja na  mbinu za uangalizi,”,amesema Peter.

Pia amesema,wamejikita kuwezesha walimu wa shule za Serikali ili kutoa wigo mpana wa wazazi kuwapeleka watoto wao shuleni  kwa kupunguziwa gharama na kuondoa kilio cha kupata haki ya msingi ya elimu kwa watoto hao na wataweza kutimiza ndoto zao pamoja na kupata fursa sawa kama wengine.

Mradi wa Wezesha Mtoto, unaotarajiwa kukamilika mwaka 2027, unalenga kuona watoto wenye changamoto ya kichwa kikubwa na mgongo wazi wakiandikishwa rasmi katika shule za Serikali na wakitimiza ndoto zao za masomo huku akitolea mfano kijana wenye  mgongo wazi wa miaka 19, ambaye ajapata fursa ya elimu kutokana na changamoto hiyo.

“MWADETA inaamini kuwa kupitia mafunzo kwa walimu na uboreshaji wa mazingira ya shule, kilio cha watoto hawa kukosa elimu kitaanza kupungua nchini,”amesema Peter.

Ofisa Elimu Maalumu Idara ya Elimu Awali na  Msingi wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu,James Mgabo,amesema,katika Halmashauri hiyo ina shule jumuishi 46 yenye wanafunzi wa mahitaji maalumu  mbalimbali 280.

Kati ya shule  hizo  zenye vitengo maalum ambazo ni Itumbili  yenye wanafunzi wenye  mahitaji maalumu 105 ambayo ni ya bpppppppweni na Wita ni ya kutwa yenye wanafunzi 87 mahitaji maalumu.

Amesema kupitia MWADETA walimu 15 wa mahitaji maalumu wamejengewa uwezo ili kuhakikisha watoto wote wanapata haki ya msingi ya elimu huku wakihamasisha jamii kuhakikisha  hakuna mtoto mwenye mahitaji maalumu ambaye  amefikisha umri wa kuanza shule  anafichwa.

“Elimu kwetu ni kipaumbele,ni msingi wa kuhakikisha kila mtoto anapata elimu stahiki.Serikali imeendelea kufanya jitihada ya kuhakikisha inapunguza changamoto ya uhaba wa walimu wa mahitaji maalumu ambapo kwa mwaka huu wa fedha walimu watano wameenda masomoni kuongeza ujuzi wa namna ya kuwahudumia watoto wenye changamoto,”amesema.

Kwa upande wake Daktari Bingwa wa upasuaji wa ubongo,uti wa mgongo na mishipa ya fahamu kutoka Hospitali ya Rufaa ya Bugando,Dkt.Misso Mpeji,amesema, changamoto ya kichwa kikubwa na mgongo wazi siyo laana hivyo ili aweze kupata fursa ya elimu na nyingine wazazi wanapaswa kuwawahisha hospitali pindi anapizaluwa na changamoto hizo.

 “Ukiwahi mtoto akapata matibabu mapema kuna uwezekano wa kufanya mambo mbalimbali ikiwemo fursa ya kielimu kwani ubongo unakuwa haujaumia zaidi,mfano tuna vijana ambao kwa sasa wanaendelea na masomo vyuo vikuu  hii ni kutokana na kuwahishwa kupata  matibabu wakiwa wadogo,”amesema.

Amesema mgongo wazi unahusisha uti wa mgongo na mishipa ya fahamu ndio inayosumbua watoto  kwani  miguu yao inakuwa  haina nguvu na kupinda pia  hawawezi kuzuia haja,hivyo wazazi wanapaswa kuelekezwa namna ya kuondoa haja hizo na mtoto  kwani ni zoezi ambalo anaweza kufanya  mwenye akiwa shuleni au sehemu ya kijamii.

“Mtoto akiwa mkubwa baada ya kufundisha ataweza kwenda chooni   mfano kila baada ya saa  mbili au tatu kwa haja ndogo na kubwa kulingana na chakula alichokula au maji aliokunywa, anafanya zoezi la kujisafisha, hii inamfanya mtoto anakuwa msafi na kuzuia kupata vidonda kwani haja ndogo ina chumvi hivyo anapoloana loana inakuwa siyo salama kwa afya yake,”amesema Dkt.Misso.

Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi jumuishi ya  Itumbili,Alice Wang’ombe,amesema,wamekuwa wakijitahidi kutoa elimu jumuishi ili kuwasaidia wenye mahitaji maalumu kuweza kutimiza ndoto za za kielimu,akitolea mfano kuwa kwa mwaka huu watahiniwa 22 wenye mahitaji maalumu shuleni hapo walifanikiwa kufanya mtihani wa taifa wa darasa la saba kati yao 19 wamefauli huku wawili wakifeli.

Amesema katika shule hiyo walikuwa na watoto wenye vichwa vikubwa watatu ambao awali baada ya kufika shuleni hapo walikuwa wanatambaa ila kama shule wakifanya jitihada za kuhakikisha wanapata vitu mwendo vilivyowasadia kutembea pia iumdombinu ni rafiki ya kuwawezesha  mwenye mahitaji maalumu kupata haki ya  elimu.

 Pia amesema,wanao walezi ambao wamefundishwa kwa ajili ya kuwasaidia watoto wenye changamoto ya kutoa haja bila kujua na wamekuwa wakushirikiana na wazazi kuhakikisha wenye changamoto hiyo wana vaa “diaper”.

Ofisa Ustawi wa Jamii Halmashauri ya Wilaya ya Magu,Coretha Sanga, ameiomba MWADETA kwenda mbali zaidi kwa utoaji wa elimu hiyo isiishie kwa walimu iwafikie wazazi ili waweze kuwapeleka watoto wao shule.