March 26, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mvua iliyoambatana na upepo mkali yaezua mapaa  na kubomoa nyumba Musoma

Fresha Kinasa TimesMajira Online Mara.

MVUA kubwa iliyonyesha ikiambatana na  upepo mkali na ngurumo za radi usiku wa kuamkia Machi 24, 2025, Katika Manispaa ya Musoma Mkoa wa Mara imesababisha athari kwa Wananchi Wanaoishi mitaa ya Amri Abeid, Shaban na Makongoro kwa kuezua mapaa ya nyumba zao, kubomoa na kujeruhi baadhi ya Wananchi ambao wamepelekwa hospital kupata huduma.

Pia mvua hiyo imeezua  mapaa ya baadhi ya Majengo ya shule ya Msingi Mwembeni, baadhi ya Majengo ya Uwanja wa Ndege Musoma, kituo cha  mafuta, nyumba za biashara, msikiti sambamba na kuathiri miundombinu ya Umeme katika baadhi ya Taasisi za Umma kupelekea  kukosa huduma pamoja na nyumba za Wananchi kukosa nishati hiyo.

Mkuu wa Wilaya ya Musoma Juma Chikoka akiwa ameambatana na Kamati ya ulinzi na Usalama ya Wilaya hiyo leo, Machi 24, 2025  wametembelea maeneo yote yaliyoathiriwa na kuwapa pole  Wananchi wote waliokumbwa na kadhia hiyo na kusema kuwa, serikali ya Wilaya hiyo inaendelea kufatha tathmini kubaini ukubwa wa  madhara yaliyosababishwa na mvua hiyo na  taarifa itatolewa. 

Pia,Chikoka amewataka Wananchi kuwa watulivu wakati huu ambao serikali iko pamoja nao kwa karibu kuhakikisha tathmini inafanyika kwa umakini. Huku akiwaomba kuendelea kuchukua tahadhari za kiusalama wakati huu ambao mvua zinanyesha.

Kwa upande wake Meneja wa TANESCO Mkoa wa Mara Mhandisi Nickson Babu  amesema, Shirika hilo kwa sasa linafanya  tathmini ya maeneo yaliyoathiriwa na kurejesha huduma ya umeme haraka hasa maeneo ya Taasisi za umama na Nyumba za  makazi ya watu.

“Niwape pole Wananchi ambao ni wateja wetu kwa madhara yaliyotokea, nguzo zimeanguka. Tunafanya juhudi kurejesha umeme maeneo yote ya Taasisi za umama na baadaye nyumba za Wananchi kuweka nguzo zilizoanguka,   niwaombe Wananchi wasiguse nyaya ama nguzo ambazo zimeanguka pia  wasiwashe  vyombo vya moto majumbani kipindi hiki ambacho tupo  katika matengenezo ya kurejesha miundombinu iliyoangika kwa ajili ya usalama.” amesema Babu.

Kwa upande wao  baadhi ya Wananchi ambao nyumba zao zimebomoka, wameiomba serikali kuwasaidia kupata makazi ya muda wakati huu baada ya makazi yao kubomoka. 

“Nachomshukuru Mungu hakuna madhara ambayo yametokea yakihusisha afya yangu ama Watoto wangu, Nyumba imeezuliwa paa upande mmoja imebomoka lakini tupo salama.Serikali itusaidie maana vyombo vyangu, magodoro yapo  nje.”amesema Neema Justine Mkazi wa Mtaa wa Amri Abeid. 

Shaban Paul Mkazi wa Mtaa wa Amri Abeid amesema kuwa, Jambo la kumshukuru Mungu mvua hiyo haijaleta madhara ya kugharimu maisha ya Wananchi.  Huku akiomba Wananchi kuzingatia ushauri unaotolewa na Serikali ikiwemo kuhama maeneo ya mabondeni na nyumba ambaza zimejengwa bila kuzingatia ujenzi bora.