Na Allan Ntana, Uyui
ZAIDI ya nyumba 500 za wananchi wa kata za Kizengi na Loya katika Halmashauri ya Wilaya ya Uyui mkoani Tabora zimeanguka na kusababisha zaidi ya kaya 900 kukosa makazi huku hekari zaidi ya 500 za mpunga zikizama na maji kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha mkoani Tabora.
Wakizungumza na gazeti hili kwa masikitiko wakazi wa kata hizo walieleza kuwa, mvua kubwa iliyonyesha mfululizo imewasababishia hasara kubwa hali iliyopelekea uharibifu mkubwa wa nyumba na mali zao.
Mzee Humud Mohamed na Juma Athuman walisema kuwa, mvua hiyo imebeba kila kitu hivyo kuwafanya waishi kwa shida na hofu kubwa katika makazi yao, waliomba serikali na wadau wengine wa maendeleo kujitokeza kuwasaidia kwani hawana hata makazi ya kuishi baada ya nyumba zao kusombwa na maji.
Baadhi ya viongozi wa serikali ya kijiji cha Mwamabondo katika Kata ya Loya walieleza kuwa, serikali ya kijiji hicho imechukua hatua kadhaa kuwasaidia wahanga ikiwemo kuwapatia makazi ya muda katika majengo ya shule wakati taratibu nyingine zikiendelea kufanyika.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya hiyo, Gift Msuya alisema kuwa, tayari juhudi za kuwanusuru wahanga wa mafuriko hayo zimeshaanza kuchukuliwa na kutoa wito kwa wadau wengine kujitokeza kuwasaidia .
More Stories
Maofisa Watendaji watakiwa kufanya kazi kwa weledi
Muhoji Sekondari kumaliza changamoto ya umbali kwa wanafunzi Musoma vijijini
Tanzania mwenyeji mkutano wa nishati wa Wakuu wa Nchi za Afrika