November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dkt. Agnes Kijazi.

Mvua kubwa kuanza kutikisa leo

Na Penina Malundo

MAMLAKA ya Hali ya Hewa Nchini (TMA),imetoa tahadhari ya kunyesha kwa mvua kubwa ndani ya siku nne kuanzia leo.

Akitoa tahadhari ya mvua hiyo jijini Dar es Salaam  jana, Meneja wa
Kituo Kikuu cha Utabiri wa Mamlaka hiyo, Samwel Mbuya, alisema mvua hiyo inatarajia kunyesha kati ya Aprili 17 hadi 20 mwaka huu.

Amesema maeneo yanayotarajia kupata vipindi vya mvua kubwa ni  Mkoa wa Pwani, Kisiwa cha Mafia, Tanga ,Dar es Salaam pamoja na Visiwa vya Unguja na Pemba.

“Tunatarajia maeneo hayo yatakuwa katika hali ya tahadhari ya kuwa na mvua kubwa hususani siku ya Jumamosi na Jumapili, na kuwepo kwa vipindi vya mvua kubwa zaidi zinatarajia kujitokeza katika baadhi ya maeneo haya,”amesema Mbuya

Amesema maeneo haya yanaendelea kupata vipindi vya mvua kubwa kwa takribani siku nne zilizopita na kwa sasa mvua nyingine ndani ya siku nne nayo inatarajia kunyesha.

Mbuya alisema wananchi wanapaswa kuchukua tahadhari zinazostahiki ili kupunguza athari ambazo zinaweza kujitokeza katika maeneo hayo.

“Pia wananchi hao wanatakiwa kuhakikisha wanazingatia maelekezo
yanayotolewa na mamlaka husika kuhusiana na ubora wa kupunguza athari za mvua hizi zinazotarajiwa kunyesha,”alisema na kuongeza;

“Mvua hizi pia ni sehemu ya mvua za masika ambazo zilianza mwezi Machi na zinaendelea katika maeneo ya ukanda wa Pwani na maeneo mengine nchini,”alisema Mbuya