Na Israel Mwaisaka, Timesmajira Online,Nkasi
Nyumba 29 zimebomoka na nyingine zikiezuliwa paa,baada ya mvua ilioambatana na upepo mkali kunyesha katika vijiji vya Mabatini na Mkangale Kata ya Namanyere huku familia kadhaa zikiachwa bila ya makazi.
Diwani wa Kata ya Namanyere Nestory Kaloto, akitoa taarifa mbele ya Kamati ya Maafa ya Wilaya ya Nkasi ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya hiyo,Peter Lijualikali, amesema tukio hilo limetokea juzi jioni,baada ya mvua iliyokuwa imeambatana na upepo mkali kunyesha na kusababisha maafa hayo.

Amesema wananchi wengi wao wanahifadhiwa kwa majirani na wanahitaji msaada wa haraka ili kuweza kurudia katika hali ya kawaida.
Mkuu wa Wilaya ya Nkasi, Peter Lijualikali, amewataka wakazi wa eneo hilo kupanda miti ya kutosha, ili kukabiliana na changamoto hiyo huku akiiagiza Halmashauri kupeleka miche ya miti mbalimbali ili waanze kuipanda.
Pia amewataka kufuata kanuni za ujenzi pale wanapoanza kujenga nyumba,ili kuweza kujenga nyumba zenye ubora zinazoweza kukabiliana na changamoto kama hizo pamoja na dhoruba.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi,Mayuma Zilantuzu,amesema kuanzia kesho miche ya miti itafika katika eneo hilo,ili watu waendelee kuipanda miti hiyo hasa katika kipindi hiki cha mvua za masika.

Awali baadhi ya waathirika wa mvua hiyo wameiomba Serikali ione namna ya kuwasaidia haraka kwani hali zao siyo nzuri,kutokana na vitu vyao vingi kuharibiwa baada ya nyumba zao kubomolewa.
Hata hivyo kamati hiyo ya maafa ilikabidhi msaada wa vifaa vya ujenzi kwa muathirika wa moto Beatrice Makoloka, mkazi wa Mabatini ambaye nyumba yake iliungua kutokana na hitilafu ya umeme.Vifaa hivyo ni mbao 15 zenye thamani ya shilingi 10,500,misumari Kg 5,saruji mifumo 4 pamoja na bati 8 ambapo vyote vina thamani ya Tshs,370,000.

More Stories
Wananchi waaswa kutoa taarifa vitendo vya ukiukwaji haki za binadamu
Tanesco,Kanona wakutana kwa mazungumzo ya awali ya biashara ya mauziano ya umeme
Wizara ya Nishati yataja mafanikio utekelezaji majukumu 2024/2025