*Waziri Mkuu kuweka jiwe la msingi mradi wa ujenzi wa vituo vya kusukuma maji,matenki
Judith Ferdinand, Timesmajira Online-Mwanza
Waziri Mkuu, wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Mwigulu Nchemba, anatarajia kuzindua safari za kibiashara za meli mpya ya kisasa ya MV. New Mwanza pamoja na kukagua miradi miwili ya maendeleo chini ya Wizara ya Uchukuzi na Wizara ya Maji.
Akizungumza waandishi wa habari, Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, alisema Dkt. Mwigulu atazindua rasmi meli hiyo itakayoanza kutoa huduma za usafiri wa abiria na mizigo kati ya Mwanza na Bukoba mkoani Kagera.
Profesa Mbarawa alisema kukamilika kwa ujenzi wa MV.New Mwanza ni utekelezaji wa Ilani ya CCM na sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuboresha usafiri wa majini, hususani kwa wakazi wa mikoa ya Kanda ya Ziwa.
Alisema meli hiyo yenye uwezo wa kubeba abiria 1,200, tani 400 za mizigo na magari 30, imekamilika kwa asilimia 100, ikiwa na urefu wa mita 92.6,upana wa mita 17 na kimo cha sawa na ghorofa nne.
“Mradi huu umegharimu kiasi cha bilioni 120.562,ambapo Serikali ya awamu ya sita ilipoingia madarakani, mradi ulikuwa umefikia asilimia 40. Kupitia uongozi wa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan, zaidi ya shilingi bilioni 79 zilizokuwa zimebaki kukamilisha mradi huu, zilitolewa,” alisema Profesa Mbarawa.
Aliongeza kuwa meli hiyo ilianza safari za majaribio Machi mwaka jana na kufanya safari sita kati ya Mwanza na Bukoba kupitia Kemondo, ikisafirisha abiria 7,028 na tani 673 za mizigo.Huku Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) likifanya ukaguzi wa ufanisi wa meli wakathibitisha ubora na usalama wake kabla ya kuruhusu safari za kibiashara kuanza.
Pia amesema, meli hiyo ya kisasa itachangia kuboresha usafiri Kanda ya Ziwa, iko katika ubora uliosanifiwa, ni salama kwa safari za abiria na mizigo.
Profesa Mbarawa alisema Serikali imewekeza zaidi ya bilioni 180 katika kuboresha miundombinu ya usafiri wa majini ndani ya Ziwa Victoria, ikijumuisha uboreshaji wa Bandari za Bukoba, Kemondo na Mwanza Kaskazini pamoja na ujenzi wa MV.New Mwanza.
Alieleza kuwa,bilioni 19.54 zimetumika kuboresha Bandari ya Bukoba, Kemondo bilioni 20 na Mwanza Kaskazini bilioni 18.6 ambapo uboreshaji wa bandari hiyo umefikia asilimia 75 huku bilioni 120 zikitumika kujenga meli ya MV.New Mwanza.
“Nitakuwa mwizi wa fadhila nisipomshukuru Rais Samia.Serikali imetoa kipaumbele kwa sekta ya uchukuzi, sh. trilioni 10 ni kwa ajili ya bandari tu na SGR trilioni 28, hivyo tunamshukuru Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuleta maendeleo katika miundombinu,”alisema Profesa Mbarawa
Baada ya uzinduzi wa meli hiyo, Dk. Mwigulu atatembelea Kituo cha Ukarabati na Uokozi cha Kimataifa kilichopo wilayani Ilemela, ambapo atakagua hatua za ujenzi, mitambo ya uokoaji, mifumo ya uratibu na uwezo wa kitaalamu wa utafutaji na uokoaji katika Ziwa Victoria.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Meli Tanzania (TASHICO), Eric Hamiss, alisema ongezeko la gharama za ujenzi wa meli hiyo kutoka bilioni 89 hadi bilioni 120 ulilitokana na athari za UVIKO-19, kupanda kwa bei ya malighafi ya ujenzi.
Alisema baada ya uzinduzi, TASHICO itatangaza rasmi nauli za meli hiyo, itakayohudumia bandari za Mwanza, Kemondo na Bukoba pamoja na Port Bell nchini Uganda na Kisumu nchini Kenya.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Mohamed Salum, alisema Kituo cha Ukarabati na Uokozi Kanda ya Ziwa kimegharimu takribani Dola za Marekani milioni tano sawa na bilioni 12, fedha zilizotumika kusimika maboya, mitambo ya hali ya hewa, boti za uokoaji na matibabu.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, alisema Waziri Mkuu atawasili majira ya saa 2:00 asubuhi na kuwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kumlaki na kushuhudia uzinduzi wa miradi hiyo ya kimkakati.
Alisema katika ziara hiyo ya siku moja, Dkt. Mwigulu pia ataweka jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa vituo vya kusukuma maji,mabomba makuu ya usafirishaji maji pamoja na matenki ya kuhifadhia maji wilayani Nyamagana.

More Stories
Wanawake jumuia ya kikristo Tanzania CCT wafundana kuelekea siku ya Wanawake Duniani
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi