November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

MV Mwanza kuanza kutumika Julai ,2023

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma.

SERIKALI imesema ujenzi wa Meli ya MV Mwanza uliogharimu bilioni 108.5 umefikia asilimia 73 ambapo inatarajia kukamilika ifikapo Mei 2023 kisha kuanza kutoa huduma kwa wananchi ifikapo Julai mwakani.

Hayo yamesemwa jijini hapa leo na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni za Meli (MSCL) Eric Hamissi, wakati akizungumza na wandishi wa habari kuhusu mwelekeo wa taasisi hiyo na utekelezaji wa bajeti ya mwaka huu.

Ambapo amesema Mkandarasi ameendelea kuagiza vifaa mbalimbali vya kumalizia umbo la meli (finishing) na kwa sasa vifaa vilivyobaki ni vya malazi (accommodation), viti na vifaa vingine vya uendeshaji wa meli (navigation), vifaa vya umeme pamoja na kupaka rangi awamu ya mwisho.

Hivyo Hamissi amesema hadi sasa ujenzi wa meli hiyo umefikia hatua nzuri na mwezi huu itaingizwa katika maji kwa ajili ya ujenzi wa vitu vya ndani na kujaribu injini kama iko vizuri.

“Tunatarajia hadi kufikia Mei tano mwakani meli hiyo ikabidhiwe na ikifika julai mwakani ianze kutoa huduma. Meli hii ni kubwa kuliko meli zote zinazoelea katika maziwa makuu kwasababu itakuwa na uwezo wa kubeba abiria 1200 na tani 400 za mizigo na ina urefu wa mita 92.6 na upana mita 17 na ina ghorofa nne,”ameeleza Hamissi.

Amesema kuwa kukamilika kwa Meli hiyo italeta mapinduzi makubwa katika sekta ya usafirishaji wa njia ya maji kwasababu itaenda Uganda, Kisumu, Bukoba na maeneo mengine ambapo kutakuwa na biashara.

Aidha Hamissi amesema kuwa katika mwaka huu wa fedha serikali imeipatia MSCL sh.bilioni 111.8 kwa ajili ya kukarabati, kuendeleza na kujenga meli 11.

Amesema fedha hizo zitakarabati meli nne, kuendeleza meli tatu na kuanza ujenzi wa meli mpya nne.

Vilevile amezungumzia Ziwa Victoria ambapo amesema serikali ya awamu ya sita imedhamilia kumaliza changamoto ya usafiri kwa njia ya maji ziwa Tanganyika.

Ambapo katika mwaka huu wa fedha imetenga sh.bilioni 53 kwa ajili ya kutekeleza miradi saba iliyopo ziwa Tanganyika.

“Serikali ya awamu ya sita imeona ni vyema kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika ziwa Tanganyika ambapo imetoa sh.bilioni 53.9.Fedha hizo zitaenda kujenga chelezo ya tani 5,000 ambayo itagharimu sh.bilioni 12 kwa sababu zitajengwa meli kubwa za mizigo na makontena makubwa ambayo yatavushwa kupelekwa Zambia na Congo,”amesema Hamissi.