December 27, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Muuguzi,hawara mbaroni kwa tuhuma za mauaji Songwe

Na Moses Ng’wat, Timesmajira Online,Mbozi

POLISI Mkoa wa Songwe linamshikiria mke ambaye ni muuguzi pamoja na anayedaiwa kuwa ni hawara yake kwa tuhuma za mauaji ya mume wake.

Taarifa za uhakika kutoka vyanzo vingine na baadae kuthibitishwa na Jeshi la Polisi zinadai kuwa watuhumiwa hao ambao majina yao yamehifadhiwa kwa kuwa bado wapo kwenye uchunguzi, wanadaiwa kuhusika na kifo cha Victor Mwakapenda (41) mkazi wa Ilembo, Mjini Vwawa, Wilayani Mbozi na mwili wake kwenda kutupwa katika msitu wa Ipoloto,wilayani Mbeya Vijijini mkoani Mbeya.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Augustino Senga, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambalo amedai uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha mauaji hayo ni wivu wa kimapenzi.

Kamanda Senga amesema marehemu alitoweka nyumbani tangu Aprili 30 mwaka huu kabla ya mwili wake kuokotwa Mei 9 mwaka huu ukiwa umetupwa katika msitu wa Ipoloto huko Mbeya Vijijini.

Kamanda Senga amesema mpaka sasa wanawashikilia watu wawili wanaosadikiwa kuhusika na tukio hilo akiwepo mke wa marehemu ambaye ni mtumishi wa serikali (Muuguzi) katika moja ya Hospitali Wilayani Mbozi, pamoja na kijana mmoja ambaye ni dereva bodaboda ambapo hata hivyo hakuwa tayari kutaja majina yao kwani bado wapo kwenye uchunguzi.

“Tunawashikilia watu wawili akiwemo mke wa marehemu kwa kuwa mara ya mwisho yeye ndiye alikuwa na mumewe,” amesema Kamanda Senga.

Kamanda Senga amesema taarifa za mwili wa marehemu kuokotwa katika msitu wa Ipoloto zilitolewa Mei 9 mwaka huu katika kituo cha polisi Mbalizi mkoani Mbeya na mwili wake ulichukuliwa na kwenda kuhifadhiwa katika Hospitali ya Ifisi mkoani humo.

Ambapo Mei 29 mwaka huu ndugu wa marehemu walipata taarifa na kwenda katika Hospitali hiyo kisha kumtambua marehemu.

“Marehemu amekutwa na majeraha mbalimbali katika mwili wake ikiwemo majeraha makubwa kichwani na jicho moja kuvimba hadi kutoka,”amesema Kamanda Senga.

Balozi wa Shina namba moja, Mantengo, Ilembo, Aliki Songa, alipokuwa akiishi marehemu amekiri kuwepo mgogoro wa kifamilia kati ya marehemu na mke wake.

“Tunasikitika juu ya tukio hili, lakini kwa kuwa tayari jeshi la polisi limeanza kuchukua hatua nafikiri taarifa nyingi tutazipata huko,ameaema Balozi huyo wa shina.