Na Allan Vicent, TimesMajira Updates, Tabora
MUUGUZI wa kike katika Kituo cha Afya Igagala, Wilayani Kaliua Mkoani Tabora Hijja Badi Lema ameuawa na mwanaume anayesadikika kuwa mpenzi wake baada ya mwili wake kupatikana ukiwa umetupwa porini.
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani hapa ACP Richard Abwao amethibitisha kutokea tukio hilo Agosti 8 mwaka huu na kubainisha kuwa mwili wa marehemu ulikutwa porini majira ya saa 11 jioni katika Kijiji na Kata ya Tumbi nje kidogo ya Manispaa ya Tabora.
Alisema marehemu ambaye alikuwa amejiunga na Chuo cha cha Uuguzi cha Tabora Polytechnique kilichoko mjini Tabora kwa ajili ya kuongeza ujuzi, alitoweka tangu Julai 30 mwaka huu chuoni hapo.
Kamanda Abwao alibainisha kuwa baada ya kupata taarifa za kutoweka kwa mwanafunzi huyo ambaye pia ni mtumishi walianza uchunguzi wa haraka kuanzia chuoni hapo na kupata taarifa zilizowezesha kukamatwa watuhumiwa wawili.
Alisema kati ya waliokamatwa mmoja anasadikika kuwa ndiye alikuwa mpenzi wake na mwingine alikuwa mwendesha bodaboda aliyekuja kumchukua siku ya tukio baada ya kupigiwa simu na mpenzi wake akimdanganya kuwa anaenda kupewa fedha zake alizokuwa amemkopesha.
Aliongeza kuwa marehemu alipelekwa katika Kijiji hicho kilichoko pembezoni mwa Mji wa Tabora ambapo ndiko walikokuwa wanaisha watuhumiwa hao.
Kamanda alifafanua kuwa marehemu hakuwa na sababu ya kuhofia usalama wake kwa kuwa alijua mpenzi wake ana nia njema, lakini baada ya kufika Kijijini hapo waliingia porini na kutekeleza mauaji hayo.
Alibainisha kuwa watuhumiwa hao wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa ajili ya uchunguzi zaidi na wanatarajiwa kufikishwa mahakamani mara tu baada ya kukamilika uchunguzi.
More Stories
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba