December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mussa: Natamani kuendelea na masomo,nikipata shule ya bweni

Na Martha Fatael

“Natamani kuendelea kusoma kama nikipewa fursa hiyo tena.Nawaomba msaada nitafutiwe shule nyingine ya bweni ili nikakae huko, maana huku mtaani ninapoishi na shule niliyokuwa nasoma awali, wamekuwa wakinitania na kuninyima furaha ya kuishi,”anasimulia mtoto Ally Mussa(siyo jina lake halisi) mwenye umri wa miaka 11 mkazi wa Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro.

Msuya anasema pamoja na kuacha shule mara mbili kutokana na kejeli anazozipata kutoka kwa wanafunzi wenzie,baada ya kufanyiwa kitendo cha ukatili(ulawiti),lakini yeye bado ana nia ya kusoma ili kutimiza ndoto yake ya kuwa Mhandisi wa umeme katika miaka ya baadaye.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Moshi Shadrack Mhagama

Licha ya tukio hilo,Dawati la Jinsia na Watoto la Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro,Koplo Mary Shemahonge, anasema,kumekuwa na kukithiri kwa matukio ya ukatili kwa watoto, ambapo kwa kipindi cha Januari hadi Agosti mwaka 2024,matukio 285 ya ubakaji na ulawiti kwa watoto yaliripotiwa.

Hata hivyo maisha ni kitabu,chenye kurasa zenye magumu,furaha,huzuni na mateso.Yapo yanayoweza kuvumilika lakini hili lililomkuta mtoto Mussa,si jepesi.Kujua hayo yote ungana na Mwandishi wa Makala haya.

Akizungumza na Timesmajira Online nyumbani kwao mkoani Kilimanjaro,Mussa anasimulia kuwa,kutokana na tukio la kikatili la kingono alilokumbana nalo,limefanya safari yake ya elimu kuwa na maumivu na kukatishwa taama ya kusonga mbele tangu mwaka 2023.

“Nimeshindwa kwenda shule,kwa sababu wanafunzi wenzangu wananitania kuwa mimi ni mwanamke, natamani kama ningetafutiwa shule nyingine ya bweni nimalize elimu ya msingi na baadaye nikasome ufundi umeme, ndoto yangu ni kuwa fundi umeme,”anasema Mussa.

Anasimulia kuwa, siku ya tukio alikuwa ametumwa na mama yake kupeleka simu katika chaji,na wakati anarejea nyumbani walijitokeza vijana wawili ambao walimkamata na kumpeleka kichakani kisha kumfanyia ukatili na baadaye kumtishia kumpiga iwapo atatoa siri hiyo.

Anasema, baada ya tukio hilo kujulikana,alihamishwa kutoka shule ya msingi ya awali aliyokuwa anasomea(jina limehifadhiwa),nakuhamishiwa shule nyingine ya msingi(jina limehifadhiwa), lakini hali iliendelea ya kuitwa mwanamke na kusababisha kuacha tena shule.

“Licha ya jitihada za wazazi wangu za kunitafutia shule nyingine, hali imekuwa mbaya zaidi.Hii yote ni kutokana na aibu ninayoipata kutoka kwa wanafunzi wenzangu wanaofahamu tukio nililotendewa,sasa nimeacha shule nashinda nyumbani kila siku ,licha ya kwamba bado anahitaji kupata elimu ili kutimiza ndoto yangu,”.

Naye, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, Shadrack Mhagama,anasema kuhusu suala la Ally Mussa,aliyefanyiwa ukatili,Serikali inatambua suala hilo na mipango ya kumtafutia shule inafanyika, ili amalize elimu yake ya msingi maana tayari jitihada zilifanyika lakini tatizo limejirudia.

“Nakiri kupokea taarifa za mwanafunzi huyo,tumejipanga kupitia Idara ya Ustawi wa Jamii,tunamsihi mtoto husika pamoja na familia yake asijione mnyonge na kusahau kile kilichotokea,maana wahusika walipewa adhabu,mipango ipo ili kutafuta shule nyingine ambayo ataendelea na elimu yake,”anasema Mhagama.

“Naiomba jamii ya watanzania kunisaidia kuhama makazi yangu Kata ya Mabogini Wilaya ya Moshi,Mkoa wa Kilimanjaro,kwani mwanangu amekatishwa masomo baada ya kulawitiwa na vijana wawili wakazi wa kata hii,”anasema mama mzazi wa mtoto huyo ambaye jina lake limehifadhiwa.

Mama huyo,anasema mwanaye ambaye alikuwa darasa la sita, ameacha shule mara mbili kutokana na wanafunzi wenzake kumkejeli kwa kumuita mwanamke baada ya kupata taarifa kwamba alilawitiwa na vijana wawili ambapo mmoja kati yao ni mwanafunzi wa shule ya sekondari.

Anasema mwanaye amekatisha masomo akiwa darasa la sita katika shule hiyo,baada ya kufanyiwa ukatili kutoka kwa vijana wawili kati yao mmoja ni mwanafunzi wa sekondari.Na kudai kuwa vijana hao ni Ibrahim Bayo na Boniface Hafron, uliofanywa Mei 7,mwaka 2023 na kumsababishia maumivu makali.

Hata hivyo,mama huyo,anasema vijana husika,walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Moshi katika kesi ya jinai namba 10 ya mwaka 2023, ambapo mahakama iliwatia hatiani na kuwapa adhabu ya kutandikwa viboko sita kila mmoja.

“Mwanangu alistahili kumaliza elimu ya msingi mwaka huu wa 2024,lakini yupo nyumbani kutokana na kushindwa kuhimili kejeli kutoka kwa wanafunzi wenzake wakiwa nyumbani na hata mtaani.Ninaomba jamii ya watanzania kunisaidia nihame Kata ya Mabogini, mtoto wangu hayuko huru,walawiti licha ya kuadhibiwa na Mahakama bado wapo mtaani,huku jamii nayo ikimkejeli mwanangu, sasa ameshindwa kusoma, nini hatma yake,”anasema.

Hata hivyo,jambo hilo linahitaji nguvu ya Serikali na vyombo vya dola,kwa kuhakikisha adhabu kwa wanaokutwa na hatia ya ukatili iwe kubwa ili iwe fundisho kwa wengine.

Mmoja wa wakazi wa kijiji cha Mji Mpya, kitongoji cha Jitengeni Kata ya Mabogini, Boniventura Kilinzi,anasema ukatili huo kwa baadhi ya vijana hujifunza kupitia mitandao na kufanya majaribio kwa watoto wenzao.Hivyo
kuna haja ya jamii kuelezwa athari za matukio ya kikatili kwa baadaye. ili kupunguza vitendo hivyo.

Ofisa Mtendaji wa kijiji cha Mabobini, Mary Adam Mkonte, amekiri kuwapo kwa matukio mengi ya ukatili ikiwemo ubakaji,ulawiti kwa watoto na wanawake pamoja na utelekezwaji wa familia, jambo ambalo linadumaza shughuli za maendeleo.

Anasema kijiji hicho kina wakazi zaidi ya 16,000,na matukio mengi hayaripotiwi inavyotakiwa,ambapo kwa mwaka yanakadiriwa kutokea matukio zaidi ya 20 lakini yanayoripotiwa ni mawili pekee.

Pia anasema,asilimia kubwa ya matukio yanashindwa kuendelea katika vyombo vya sheria kutokana na wahusika wa matukio hayo kuwa ndugu wa familia kama baba,mjomba,kaka,babu na ndugu wengine.Ambapo kesi huripotiwa katika hatua za awali,lakini baadaye humalizwa kwa vikao vya kifamilia ama hupokea fedha ili kumaliza kesi hizo.

Sanjari na hayo, anasema usalama wa watoto kijijini hapo siyo shwari, kwani asilimia kubwa ya familia hizo zinasimamiwa na mzazi mmoja, ambaye anajishughulisha kutafuta fedha za kuwahudumia na malezi, hivyo hutumia muda mwingi kwenye shughuli za utafutaji fedha kuliko za malezi ya watoto.

Hata hivyo Mkonte anatoa tahadhari kwa wazazi na walezi kuongeza umakini kwenye uangalizi wa watoto,kwa kuwakagua mara kwa mara kwani matukio mengi ya ukatili kwa watoto hutokea ndani ya familia ikilinganishwa na nje ya familia na shule.

Amesema kijiji kwa kushirikiana na wadau likiwemo Dawati Jinsia na Watoto la Jeshi la Polisi,watoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa kukaa karibu na watoto wao ili kujua changamoto na kuwakagua kama wamefanyiwa ukatili wa aina yoyote.

Kuhusu changamoto ya watoto kutembea umbali mrefu kwenda shule hususani eneo la Shabaha,anasema suala hilo linafanyiwa kazi na Serikali ili kuwaondoa changamoto na vishawishi vinavyowasababishia watoto,kufanyiwa ukatili.

Naye, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, Shadrack Mhagama, anasema baadhi ya matukio ya ukatili yanasababishwa na watoto kutembea umbali mrefu,ambapo kwa sasa wanafunzi wanaoshi eneo la Shabaha,wantembea umbali mrefu kufuata elimu katika shule za msingi Benjamin Mkapa, Mabogini na Muungano.

“Juhudi zinafanyika za kujenga shule katika Kjiji cha Shabaha,ambapo Serikali imetoa tangazo kwa wananchi wa eneo hilo kujitolea mashamba yao ama kutafuta eneo ambalo watu watalipwa fidia,ili kutenga ardhi kwa ajili ya ujenzi wa shule,”.

Anasema ili kuongeza ulinzi kwa watoto ni lazima kuwe na ushirikiano wa karibu baina ya walimu, walezi, wazazi na jamii,ili kuhakikisha wakati mwanafunzi yupo njiani kuelekea ama kutoka shule, pande hizo mbili zinawasiliana na kukabili baadhi ya watu wasiokuwa na nia njema.

Akitoa ufafanuzi wa matukio yanayoendelea,Ofisa kutoka Dawati la Jinsia na Watoto,Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Koplo Mary Shemahonge,wamekuwa wakitoa elimu kwa jamii,kuhusu kuzuia matukio ya ukatili, kutoa taarifa pindi yanapotokea matukio hayo,pamoja na ushirikiano wakati kesi husika zinapofikishwa mahakamani.

Anasema miongoni mwa mbinu za kukabili ukatili kwa watoto ni pamoja na kuimarisha uhusiano baina ya watoto na wazazi ikiwa ni pamoja na watoto kupata chakula cha mchana shuleni ili kupunguza vishawishi ambavyo vnaweza kusababisha akafanyiwa ukatili baada ya kupewa zawadi.

Anasema maeneo ya vijijini na pembezoni mwa mji,ndio yenye changamoto kubwa ya vitendo vya ukatili kwa watoto na wanawake,kama vile Mabogini na Kibosho Halmahauri ya Wilaya ya Moshi, Rombo, Hai na maeneo ya Manispaa ya Moshi katika Kata za Pasua, Njoro na Majengo.