January 10, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Muslimu atembelea majeruhi Asas atoa pole ajali Iringa

Na Zuhura Zukheir, TimesMajira Online, Iringa

KAMANDA wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini Kamishna Msaidizi wa Polisi Fortunatus Muslimu ametembelea majeruhi wanaoendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa baada ya kujeruhiwa katika ajali ya basi la abiria Kampuni ya Prezdar iliyotekea milima ya Kitonga mkoani Iringa

Kamanda Muslimu amesema basi hilo lenye naomba za usajili T326 CSX Kampuni ya Prezdar linalofanya safari zake Iringa – Dar es salaam liliatumbukia katika maporomoko ya Milima ya Kitonga wilayani Kilolo.

Kamanda Muslimu aliwataka madereva kutambua kuwa wamebeba roho za watu hivyo wanatakiwa kuchukua tahadhari muda wote wanapokuwa barabarani.

Amesema Jeshi la Polisi litaendelea kusimamia sheria za usalama barabarani kwa kuwachukulia hatua madereva wote wanaoonekana kuvunja sheria.

Amesema jeshi hilo pia linaendelea kumtafuta na kumfikisha katika vyombo vya sheria dereva wa basi hilo ambaye alitokomea kusikojulikana mara tu ilipotokea ajali.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama Barabarani Salim Abri Asas ametoa pole kwa wafiwa wote huku akiwatakia uponyaji wa haraka majeruhi wanaoendelea kupatiwa matibabu hospital.

Asas ameliomba Jeshi la Polisi kumtafuta na kumkamata dereva huyo aliyekimbia baada ya kutokea kwa ajali hiyo iliyosababisha vifo na majeruhi 

Amesema kitendo cha dereva huyo kutokomea kusikojulikana inaaminisha kuwa ajali hiyo ilikuwa ni ya makusudi kwakuwa angekuwepo angetoa ushirikiano mzuri kwa mamlaka zinazohusika

“Huyu dereva ni muuaji haiwezekani iwe ajali ya bahati mbaya harafu akimbie badala ya kutoa ushirikiano kwa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama ningeomba wenzetu wa polisi wamtafute wamkamate na afikishwe katika vyombo vya sheria” amesema Salim Asas.

Watu 10 wamepoteza maisha na wengine 50 wamejeruhiwa katika ajali hiyo huku miili 5 ikiwa tayari imetambuliwa na ndugu zao.