March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mume atuhumiwa kumuua mke mjamzito kwa  kipigo

*Inadaiwa kumshambulia kwa ngumu, mateke sehemu mbalimbali za mwili

Judith Ferdinand, Timesmajira Online-Mwanza 

Seke Sesila(45),mkazi wa kitongoji cha Tinda,Kata ya Mwamabanza, wilaya ya Magu mkoani Mwanza  anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za mauaji ya mke wake aitwaye Rahel Mabina(39) mkazi wa kitongoji hicho.

Inadaiwa kuwa marehemu Rahel,aliuawa kwa kushambuliwa kwa ngumi na mateke sehemu mbalimbali za mwili wake.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Wilbord Mutafungwa,amesema tukio hilo limetokea Januari 15,2026, majira ya 1.00 asubuhi,kitongoji cha Tinda,kijiji na kata ya Mwamabanza, wilaya ya Magu, baada ya kutokea kwa ugomvi wa kifamilia baina yao.

Ambapo mtuhumiwa Seke alimshambulia mke wake ambaye alikuwa na ujauzito wa miezi miwili kwa mateke na ngumi sehemu mbalimbali za mwili wake ikiwemo tumboni hali iliyo sababisha kupoteza nguvu na hatimae kufariki.

“Taarifa kuhusiana na tukio hili zinaonesha kuwa marehemu alikuwa mke wa tatu wa mtuhumiwa na wamebahatika kupata mtoto mmoja. Chanzo cha tukio hili ni mgogoro wa kifamilia uliotokana na marehemu kudai fedha ya matumizi kwa mume wake,”amesema Mutafungwa.

Mutafungwa amesema,mwili wa marehemu umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti Hospitali ya wilaya ya Magu kwa uchunguzi wa kitaalam.

Huku mtuhumiwa anaendelea kuhojiwa na upelelezi utakapo kamilika atafikishwa mahakani kwa taratibu za kisheria.

Hata hivyo amewaasa wananchi kujiepusha na vitendo vya ukatili wa kijinsia na badala yake wakumbuke kufanya mazungumzo yatakayoleta maelewano katika familia hizo ili kuepuka matukio ya mauaji.