Na Mwandishi Wetu,Timesmajira Online.
WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Afrika Kusini, Grace Naledi Pandor kujadili mambo ya kuendeleza mashirikiano baina ya nchi hiyo na Tanzania.
Balozi Mulamula, amefanya mazungumzo hayo Pretoria nchini Afrika Kusini ambapo amesema mahusiano kati ya Afrika Kusini na Tanzania ni ya kihistoria na yameendelea kuimarika tangu enzi za kupigania uhuru kwa nchi za Kusini mwa Afrika.
Kwa upande wake Waziri Pandor, ameshukuru kwa ujio wa Balozi Mulamula na kwa kufika nchini Afrika Kusini na pia ameeleza kuwa nchi yake, inathamini mashirikiano ya kihistoria kati ya nchi hizo mbili na hivyo kinachohitajika ni kuendeleza na kuimarisha mashirikiano ya kiuchumi na kisiasa yaliyopo.
Amesema Afrika Kusini ina azma ya kushiriki kikamilifu kujenga makumbusho ya urithi ya harakati za kupigania uhuru Kusini mwa Afrika, zenye chimbuko lake nchini Tanzania na vilevile kuonesha juhudi za Tanzania katika harakati za kupigania uhuru na kwa nchi za Kusini mwa Afrika.
Wamejadili pia mchakato wa tathmini ya utekelezaji wa Bi-National Commission (BNC), ambapo kwa mwaka huu Afrika Kusini ndiyo itakuwa mwenyeji wa tathmini hiyo ambayo hujumuisha ngazi ya watedaji wakuu wa sekta mbalimbali wa nchi hizo mbili, Mawaziri na huitimishwa na Marais wa nchi zote mbili.
Balozi Mulamula kabla ya kukutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini, amekutana na watumishi wa Ubalozi wa Tanzania Pretoria katika mkutano ulifanyika Ubalozini.
Katika kikao hicho amepokea taarifa ya eneo la uwakilishi la Ubalozi ambalo linajumuisha Afrika Kusini, Botswana, Falme ya Lesotho na SADC.
Taarifa hiyo imeeleza juhudi za Ubalozi katika kukuza mahusiano na nchi za eneo la uwakilishi, ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa diplomasia ya uchumi, diplomasia ya siasa na wanadiaspora wa eneo la uwakilishi.
Balozi Mulamula ameutaka Ubalozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, kuendela kufanya kazi kwa malengo na watumishi kujiwekea malengo ili kufanikisha malengo ya Ubalozi na hatimaye Ubalozi, kuchangia malengo ya Wizara kwa ujumla.
“Nawasihi kuendeleza mahusiano na nchi za uwakilishi na Balozi nyingine zilizopo katika nchi za uwakilishi na suala hili la kujenga mahusiano na watumishi wote na si Balozi pekee yake,” amesema.
More Stories
Chunya yafikiwa na Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano
HGWT yawarejesha kwao wasichana 88 waliokimbia ukeketaji
Sherehe Miaka 61 ya Mapinduzi Zanzibar zafana