Na Yusuph Mussa, TimesMajira Onlinnne, Korogwe
SHEIKH Mkuu na Mufti wa Tanzania Dkt. Aboubakar Zubeir Bin Ally Mbwana amewataka wananchi na viongozi wa Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga kumpa ushirikiano Mkuu wa Wilaya hiyo Jokate Mwegelo.
Amesema ana uzoefu na viongozi na wananchi wa wilaya hiyo sababu na yeye Korogwe ni nyumbani, huwa wanakwenda mkoani Dodoma yalipo Makao Makuu ya Serikali, kufanya ushawishi ili viongozi wasiowataka wahamishwe ama kuondolewa kwenye wilaya hiyo.
Aliyasema hayo Aprili 19, 2023 kwenye hafla ya Iftar na dua ya kumuombea Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, na kufanyika mjini Korogwe, na kuongeza kuwa kwa uwezo alioonesha Jokate tangu amekwenda Wilaya ya Korogwe, ataweza kuwafikisha mbali.
“Wananchi na viongozi wa Korogwe naomba tumlinde, tumtumie na kuona anafanya kazi. Tuache kwenda Dodoma mara kwa mara, na ninaposema hivyo, wengi mnanielewa. Tumpe nafasi ya kututumikia, na kama ninavyosema kwenye kauli mbiu yangu, tujitambue, tubadilike, tuache mazoea.
“Niendelee kusisitiza, tutakuheshimu, tutakunusuru. Ninaposema tutakunusuru, wengi wanafahamu. Korogwe tuna mengi ya kufanya, hivyo tunahitaji mtu kama wewe (Jokate) aweze kutusaidia. Wananchi wamekuwa wanalima mahindi na maharage bila mafanikio, sasa umefika wakati wa kutumia dhahabu nyeupe ya Mkoa wa Tanga ambayo ni mkonge. Hivyo wananchi wahimizwe walime mkonge” alisema Mufti.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe Ali Mkomwa ambaye alialikwa kwenye Iftar hiyo, alisema Jokate amefanya makubwa kwenye Wilaya ya Kisarawe japo alikuwa ndiyo anaanza kuwa Mkuu wa Wilaya.
“Alianzisha Tokomeza Zero ikiwa ni jitihada zake kuona watoto wanasoma hasa wale wa kike. Na kuna Shule ya Sekondari ya Wasichana ina kidato cha kwanza hadi cha sita inaitwa Jokate Mwegelo kwa ajili ya heshima yake baada ya yeye mwenyewe kushiriki kuijenga kwa asilimia 100. Hivyo, sio Korogwe tu ambapo ni karibu, hata angepelekwa Shinyanga tungekwenda” alisema Mkomwa ambaye aliongozana na viongozi wengine wa Kisarawe.
Katibu wa CCM Mkoa wa Tanga Selemani Mzee, alisema kwa muda mfupi, Jokate ameweza kuleta utulivu kwa viongozi wote wilayani Korogwe, na hivyo kuweza kuchochea maendeleo kwa wananchi, huku akimtaka afanye kazi ya kuwasaidia wananchi wa Korogwe, na wao CCM wapo pamoja nae na wanamuunga mkono.
Jokate, alitumia hafla hiyo ya Iftar kujitambulisha huku akimshukuru Rais Dkt. Samia kwa kumteua kuwa Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, na kuahidi atafanya kazi kwa ushirikiano kuanzia kwa viongozi wa wilaya, halmashauri, tarafa, kata, vijiji, mitaa na vitongoji hadi wananchi, ili kuweza kuharakisha shughuli za maendeleo.
“Naomba ushirikiano wenu. Nipo tayari kujifunza na kushirikiana ili mradi kuona wananchi wanapata maendeleo. Korogwe ina mambo mengi makubwa. Korogwe kuna sehemu ya kuweka Bandari Kavu. Na hiyo inawezekana sababu mkonge ndiyo zao linalopitishwa kwa wingi kwenye Bandari ya Tanga.
“Na bado, mkonge mwingi unatoka Wilaya ya Korogwe, hivyo tukiweka Bandari Kavu kilomita 100 kutoka ilipo bandari, Korogwe tutapata manufaa makubwa kwa ajili ya zao letu la mkonge” alisema Jokate.
Katika Iftar hiyo, zawadi mbalimbali za vyakula ilitolewa kwa makundi maalumu kwa ajili ya Sikukuu ya Eid El- Fitr, na itawanufaisha wananchi zaidi ya 500 wa Wilaya ya Korogwe. Ni baada ya kutolewa na Rais Dkt. Samia. Zawadi hizo ni mchele, ngano, sukari, mafuta ya kula, sabuni za unga, na baadhi ya miswala kwa ajili ya kuswalia, ilitolewa kwa misikiti zaidi ya 10.
More Stories
Rehema Simfukwe atoboa siri sababu kuimba wimbo wa Chanzo
Tanzania ipo tayari kupokea wakuu wa nchi,mkutano wa nishati-Dkt.Kazungu
Chunya yafikiwa na Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano