Na Mwandishi wetu, Timesmajira
Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Bw. Lazaro Twange amesema Mradi wa uzalishaji umeme unaotokana na jua wa Kishapu Mkoani Shinyanga umefikia asilimia 63.3 kukamilika ambapo amesema awamu ya kwanza ya Mradi huo utazalisha Megawati 50 ambazo zitaingizwa kwenye gridi ya Taifa ifikapo mwishoni mwa mwezi wa kumi mwaka huu.
MD Twange ameyasema hayo leo Juni 8 mwaka 2025 alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya mradi huo ambao unagharimu kiasi cha shilingi Bilioni 118 kwa awamu ya kwanza huku awamu ya pili ikitarajia kutumia kiasi cha shilingi Bilioni 204.
‘’Kwanza tunamshukuru Mhe. Rais kwa kutupatia fedha kwa awamu zote, kama mnavyoona kazi inaendelea na Mradi unatarajia kuingizwa kwenye Gridi ya Taifa mwishoni mwa mwezi wa kumi kwa ajili ya kuwasambazia umeme wananchi, lakini pia tuko katika hatua za mwisho za manunuzi kwa ajili ya kumpata mkandarasi atakayetekeleza Mradi kwa awamu ya pili ambayo itazalisha megati 100’’ amesisitiza Mkurugenzi Mtendaji Twange.

Aidha, amewahakikishia wananchi kuwa TANESCO inafanya jitihada za makusudi za kuhakikisha Mradi unakamilika kwa wakati ili kuendana na ongezeko la mahitaji ya watu na shughuli za uwekezaji ambazo zinategemea nishati ya umeme kujiendesha.
Naye Meneja wa Mradi huo Mhandisi Emmanuel Andarson amesema awali Mradi huo ulipaswa kukamilika mwezi February mwaka huu lakini Mkandarasi aliongezewa muda baada kukabiliwa na baadhi ya changamoto ambapo ameahidi kukamilisha Mradi huo kwa mujibu wa makubaliano ya mkataba .

Mradi wa uzalishaji wa umeme unaotokana na nguvu ya jua wa Kishapu uliopo katika Kijiji cha Ngunga Mkoani Shinyanga ulianza utekelezaji wake Desemba 8 mwaka 2023 na unatarajia kukamilika rasmi Oktoba 29 2025 ambapo unagharimu jumla ya shilingi bililioni 323 kwa awamu zote mbili ukitarajia kuzalisha megawati 150 za umeme.
More Stories
Ussi awataka wananchi Handeni kulinda miundombinu ya maji
Wapambe waanza rafu za uchaguzi Morogoro Mjini
Daraja la J.P.Magufuli kuzinduliwa Juni 19,2025