January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mtungi wa Oksijeni waua 82

BAGHDAD, Imeelezwa kuwa, moto ulioanza baada ya mtungi wa oksijeni kulipuka umeuwa watu wasiopungua 82 na wengine 110 kujeruhiwa katika hospitali mjini Baghdad nchini Iraq.

Kwa mujibu wa Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani nchini humo, Khalid al- Muhanna tukio hilo limetoke katika hospitali hiyo iliyokuwa ina vifaa vya kuwahudumia wagonjwa wa COVID-19.

“Tunahitaji kwa haraka kupitia tena hatua zote za kuhakikisha usalama katika hospitali zote kuepusha tukio kama hili la kusikitisha kutokea tena siku za usoni,”amesema Msemaji wa wizara hiyo, Khalid al- Muhanna wakati akitoa taarifa kwa umma.

Waziri Mkuu Mustafa al-Kadhimi ameagiza uchunguzi ufanyika juu ya moto huo. “Tukio kama hili ni Ushahidi wa uzembe na hivyo nimeagiza uchunguzi uanze mara moja na meneja wa hospitali na viongozi wa usalama na ukarabati wa hospitali hiyo wakamatwe pamoja na wote wanaohusika mpaka pale tutakapowatambua wale waliofanya uzembe huo na kuwawajibisha,”amesema katika tamko lake.

Wakati huo huo, Umoja wa Mataifa umeelezea mshtuko wake kufuatia vifo vya watu 82 vilivyotokea baada ya moto huo mkubwa kulipuka katika hospitali ya Ibn Khatib inayotibu wagonjwa wa COVID-19 kwenye mji mkuu wa Iraq, Baghdad.

Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Iraq, Jeanine Hennis-Plasschaert ametumia taarifa iliyotolewa mjini Baghad kutuma salamu za rambirambi kwa familia za waliopoteza maisha huku akiwatakia ahueni ya haraka majeruhi.

Mwakilishi huyo ambaye pia ni mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Iraq (UNAMI) ametoa wito kwa mamlaka kuchukua hatua thabiti kuhakikisha janga kama hilo halitokei tena.

Katika hatua nyingine. Waziri Mkuu wa Iraq, Mustafa al-Kadhimi amemsimamisha kazi Waziri wa Afya na kuagiza uchunguzi wa tukio hilo ufanyike haraka.

Amesema, Umoja wa Mataifa unaendelea kutoa msaada muhimu kwa sekta ya afya nchini Iraq wakati huu ambapo janga la Corona linazidi kushika kasi nchini humu, akiongeza kuwa Umoja wa Mataifa uko tayari kutoa msaada zaidi na kusaidia mamlaka za afya kudhibiti ugonjwa huo.

Kwa upande wake Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) kupitia mtandao wa Twitter imetuma salamu za rambirambi huku likitakia ahueni majeruhi.

Hayo yanajiri wakati ambapo nchini Iraq, ugonjwa wa Corona umekuwa mzigo mkubwa kwa mfumo wa afya ambapo hospitali zimezidiwa uwezo na takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) tangu mwezi Januari, mwaka jana 2020 hadi sasa, Iraq imekuwa na wagonjwa zaidi ya milioni moja wa Corona ambapo kati yao hao 15,217 wamefariki dunia.