Na Israel Mwaisaka, Timesmajira Online,Nkasi
MFANYAKAZI wa Benki ya NMB tawi la Nkasi wilayani Nkasi mkoani Rukwa John Maduhu (32) mkazi wa Majengo mjini Namanyere amekutwa amekufa nyumbani kwake kwa kujinyonga kwa kamba.
Akizungumzia tukio hilo Mwenyekiti wa mtaa wa Majengo Soko Kuu William Katutu ameeleza kuwa tukio hilo limegundulika Mei 10,2024 majira ya saa 3 asubuhi na wafanyakazi wa benki hiyo baada ya mfanyakazi mwenzao kutoonekana ofisini asubuhi hiyo.
Ameeleza kuwa tukio hilo liligundulika baada ya kuchungulia dirishani katika nyumba aliyokuwa akiishi marehemu ndipo walipouona mwili ukining’inia kwenye mlango wa chumbani kwake.
Mwenyekiti huyo wa mtaa amedai kuwa baada ya tukio hilo walitoa taarifa Polisi ambao walivunja mlango na kuingia ndani na kumkuta marehemu akiwa amejining’iniza  juu ya mlango wa chumbani kwa kutumia kamba ya jiko la umeme.
Ofisa Mtendaji wa mtaa huo wa Majengo Flora Mbaule amekiri kutokea kwa tukio hilo huku akidai kuwa hadi sasa haijulikani chanzo kilichopelekea kijana huyo kujinyonga kwa maana hakuacha ujumbe wowote.
Kaimu Meneja wa NMB tawi la Nkasi Marijani James amekiri kutokea kwa tukio hilo ingawa hakuwa tayari kulizungumzia kwa undani kwa kuwa yeye siyo msemaji wa benki hiyo.
Kamanda wa Polisi Mkoa Rukwa Shadrack Masija amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na ameshauri watu kuwashirikisha watu wao wa karibu pale wanapokumbana na changamoto za kimaisha badala ya kujichukulia sheria mikononi.
More Stories
AZAKI yawasilisha mapendekezo yao kwa Serikali katika kuboresha Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050
CP.Wakilyamba :Uvamizi maeneo ya hifadhi ya taifa katavi haukubaliki
Watu wawili wanaodhaniwa majambazi wapigwa risasi na Polisi