November 19, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mtumishi Halmashauri Ya Kalambo Mbaroni Kwa Kukutwa Na Mashine Bandia Ya Ukusanyaji Mapato

Na Israel Mwaisaka, TimesMajira Online, Rukwa

Jeshi la polisi Mkoani Rukwa linamshikilia Timoth Ngambeki ambae ni mtumishi wa Halmashauri ya Kalambo kwa tuhuma za kutumia mashine bandia na kutoa risiti feki kwa wananchi na kuisababishia serikali hasara ya shilling million thelathini na tisa na laki tano.

Mapema leo akizungumza use ofisini kwake mkurugenzi mtendaji Halmashauri ya Kalambo Shafi Mpenda alisema mtumishi huyo aligundulika kufanya kitendo hicho baada ya kushindwa kuwasilisha fedha Benk na kwamba baada ya ufuatiliaji zaidi kwenye mageti ya ukusanyaji mapato aligundua uwepo wa udanganyifu kwenye utoaji wa risiti.

‘’baada ya kugundua uwepo wa udanganyifu kwenye swala la ukusanyaji mapato nilianzisha utaratibu wa kuweka madaftari ya kusaini kwenye mageti yote yanayo unganisha halmanshauri za jirani na kuweka watu ambao walikuwa wakifanya kazi ya kupiga picha risiti za ushuru kisha kunitumia na wakati mwingine nilikuwa nikiamka usiku na kufuatilia mwenendo wa ukusanyaji mapato kwenye mageti.’’alisema Mpenda.

Alisema kuanzia kipindi cha mwezi juni 2023 kijana huyo alikuwa amekusanya kiasi cha shillingi million sitini na moja na laki tatu na thelathini na tano na kati ya fedha hizo kiasi cha shillingi million ishirini na moja laki nane na ishirini na tano ndizo aliwasilisha benki huku fedha kiasi cha shilling million thelathini na tisa zikiwa haizonekani zilipo.

Alisema mpaka sasa wanaendelea na ufuatiliaji ili kubaini kama kuna fedha zingine ambazo zilikusanywa na kutumika kinyume na utaratibu na kuwataka watumishi wilayani humo kuendelea kufanya kazi kwa uadilifu ili kufikia malengo ya serikali.

Kwa upande wake kamanda wa jeshi la polisi mkoani Rukwa ACP Shadrack Masija amekili kumshikilia mtumishi huyo na kusema alikamatwa na mashine mbili za ukusanyaji mapato, ambapo kati ya hizo mashine moja ikiwa ni ya bandia na nyingine ya serikali na kwamba atafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika.

Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya Kalambo mkoani Rukwa Shafii Mpenda