May 14, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mtoto wa miaka 6 afariki kwa ashambuliwa na fisi

Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza

MTOTO mmoja aliyetambulika kwa jina la Dalaile Milambo (6) mwanafunzi wa chekechea, wilayani Kwimba, mkoani Mwanza amefariki baada ya kushambuliwa na fisi.

Akizungumza jijini Mwanza, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza ACP. Muliro Jumanne amesema tukio hilo lilitojea Juni 22, mwaka huu saa moja jioni katika Kijiji cha Mwampuru Kata ya Mwantare wilayani Kwimba.

Muliro amesema mwanafunzi huyo wa shule ya chekechea ya Mwampuru alifariki baada ya kushambuliwa na fisi sehemu mbalimbali za mwili wake wakati alipokuwa na dada yake.

Amesema, mwili wa marehemu umefanyiwa uchunguzi na daktari na umekabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya taratibu za mazishi.

Hata hivyo, Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Idara ya Wanyamapori na wananchi wanamsaka fisi huyo ili adhibitiwe kwa mujibu wa sheria na kuhakikisha kuwa haleti madhara zaidi.