May 18, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mtoto mchanga, aliyedaiwa kuibwa apatikana akiwa hai

*Amekutwa ametelekezwa pembezoni mwa nyumba yao

*Baba mzazi ajaribu kumkimbiza mtuhumiwa bila mafanikio

Na Esther Macha Timesmajira , Mbeya

MTOTO wa jinsi ya kiume aliyekuwa na siku kumi na nne,mkazi wa mtaa wa Iyela One kata ya Iyela jijini Mbeya,aliyedaiwa kuibwa na mtu asiyejulikana jioni ya Aprili 29,2025, muda mfupi baada ya mama yake Neema Mkunywa kumsindikiza mgeni,amepatikana akiwa hai akiwa ametelekezwa pembezoni mwa nyumba yao Mei 15,2025 majira ya saa mbili na nusu usiku.

NeemaMkunywa,amedai kuwa siku ya tukio alitembelewa na mgeni ambaye ni dada yake,baada ya maongezi alimsindikiza umbali wa mita 300,lakini aliporejea hakumkuta mtoto ambaye alikuwa amemlaza sebuleni.

Baada ya kumkosa alimuuliza Aines Lwinga,ambaye ni mwenye nyumba wake,aliyedai kutomuona mtoto, wakamaua kutoa taarifa kwa Balozi Msaidizi,Neva Mgode ambaye alitoa taarifa kwa Mwenyekiti wa Mtaa Gabriel Button, naye akatoa taarifa polisi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa mtaa huo,Gabriel Button,amedai kusikitishwa na tukio hilo na kusisitiza kuwa ni la kwanza kutokea mtaani kwake, huku akiwataka wazazi kuwa makini na familia zao na kutowaami wageni wanaowatembelea.

Baada ya kutafutwa kwa wiki tatu bila mafanikio imedaiwa mtoto huyo alitelekezwa na mwanamke ambaye hakufahamika jina wala makazi kisha kutumia mbio.

Baba Mzazi Ambele Mwampagama,alijaribu kumkimbiza mwanamke anayedai kumuiba mtoto huyo kisha kumtekeleza , pembezoni mwa nyumba yao,lakini hakufanikiwa ndipo taarifa ilitolewa polisi ambao walifika kisha kumpeleka mtoto huyo hospitali ya rufaa ya wazazi Meta baada ya uchunguzi mtoto amekabidhiwa kwa mama yake.

Wazazi na familia kwa ujumla wamewashukuru Watanzania kwa maombi yao hata kufanikiwa upatikanaji mtoto akiwa hai.

Matukio ya wizi wa watoto mkoani Mbeya yamekuwa yakijirudia huku baadhi ya wahalifu wakikamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.