Judith Ferdinand, Mwanza
Taasisi ya Desks and Chair Foundation imeendelea kumsaidia mtoto Aristidia Bosco (17) mkazi wa wilayani Muleba, Mkoa wa Kagera aliyekuwa anasumbuliwa na uvimbe kwenye mguu wa kulia na kujitokeza kuomba msaada wa matibabu kupitia Gazeti la Majira kwa kumpatia magongo ya kutembelea pamoja na baiskeli ya magurudumu manne (wheelchair) huku ikihaidi kumsaidia mguu wa bandia.
Taasisi hiyo imetoa msaada huo leo baada ya Aristidia Bosco kufanyiwa upasuaji wa kukatwa mguu iliofanyika Mei 20 mwaka huu katika hospitali ya Rufaa ya Bugando anapoendelea kupatiwa matibabu.
Akizungumza wakati akipokea msaada huo kwa niaba ya mama mzazi wa mtoto huyo, Mwenyekiti wa Klabu ya Wandishi wa Habari Mkoa wa Mwanza(MPC) Edwin Soko, alishukuru gazeti la Majira kwa kusaidia kutangaza habari za mtoto huyo na kupelekea wadau mbalimbali kujitokeza kumsaidia na kufanikisha matibabu yake.
Soko amesema Aristidia alifanyiwa upasuaji juzi (jumatano) ili kuondoa uvimbe ambao ulikuwa kwenye mguu wa kulia, baada ya madaktari kuthibitisha kuwa alikuwa akisumbuliwa na saratani ambapo upasuaji huo ulienda salama na tayari mtoto huyo amerudishwa wodini na anendelea na matibabu.
Naye Mwenyekiti wa Desks and Chair Foundation, Sibtain Meghjee, ameshukuru kwa taarifa kuwa mtoto huyo anaendelea vizuri kinachotakiwa kwa sasa ni kumpa faraja na kumtia moyo yeye na familia yake.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa