Judith Ferdinand, TimesMajira Online,Mwanza
Mtoto mwenyewe umri wa miezi 6,aliyeibwa Machi 26, mwaka huu wilayani Sengerema mkoani Mwanza amepatikana baada ya Polisi kufanya msako na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa wa wizi wa mtoto huyo.
Akizungumzia tukio hilo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Wilbroad Mutafungwa, ameeleza kuwa Machi 26,2023 majira ya saa mbili (08:00( asubuhi, huko mtaa wa Migombani, Kata ya Nyampulukano,Tarafa ya Sengerema, kuliripotiwa taarifa ya wizi wa mtoto aitwaye Anitha Richard mwenye umri wa miezi 6 na mtu ambaye hakujulikana.
Mutafungwa ameeleza kuwa mama wa mtoto huyo aitwaye Agnes Robert, mwenyewe umri wa miaka 26, Mkazi wa Migombani alimuacha mtoto huyo kwa binti yake mdogo aitwaye Martha Richard, mwenyewe umri wa miaka 9 akiwa amembeba mgongoni kisha yeye kuingia bafuni kwa ajili ya kuoga.
Baada ya muda Martha, akiwa amembeba mdogo wake mgongoni aliitwa na jirani yao aitwaye Costancia Deonatus na kumuagiza akiwa na watoto wenzake kufuata ndoo yake kwa mtu aliyekuwa amenunua mkaa kwake ambaye jina lake halikufahamika.
Ambapo Agnes Robert ambaye ni mama wa mtoto alipomaliza kuoga alitoka na kuanza kuwatafuta watoto wake na ilipofika majira ya saa 7 (13:00) mchana watoto wawili walirejea nyumbani bila ya yule mwenzao wa miezi 6 aliyekuwa amebebwa mgongoni na dada yake, ndipo wazazi waliweza kugundua kuibiwa kwa mtoto wao na kutoa taarifa kituo cha polisi.
“Baada ya tukio hilo kuripotiwa Askari Polisi walifanya msako mkali na kufika katika kijiji cha Nyamaduke na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa Happyness William, mwenyewe umri wa miaka 18 na mkazi wa Nyehunge akiwa na mtoto huyo aliyetambuliwa na wazazi wake kuwa ndiye aliyeibiwa katika kijiji hicho,”ameeleza Mutafungwa.
Pia ameeleza kuwa baada ya mahojiano ya kina mtuhumiwa amekiri kuhusika na tukio la wizi wa mtoto huyo ambapo alidai kuwa alienda kumuonesha mumewe kuwa amejifungua.
Upelelezi wa kesi hiyo unakamilishwa mara moja na mtuhumiwa atafikishwa mahakamani haraka iwezekanavyo kukabiliana na mkono wa sheria.
Hata hivyo Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linaendelea kutoa rai kwa wazazi na walezi kuendelea kuchukua tahadhari na kutimiza jukumu lao la msingi la uangalizi wa watoto na sio kuwaacha peke yao bila uangalizi wa mtu mzima.Â
More Stories
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba
TRA kuongeza idadi ya waendesha uchumi walioidhinishwa
TRA Tanga wajivunia ukusanyaji mapato