December 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mtoto akaa siku 60 ICU, hospitali ikitumia mil 10 kumtibu

Na Raymond Mtani-BMH

Novemba 11, 2023, Bi. Janeth (35), mkazi wa Manyoni Singida, alifika Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) baada ya kukaa siku saba katika Hospitali ya Wilaya ya Manyoni akiimuuguza mwanaye aliyepatwa “degedege”.

Siku hiyo, ikawa safari ya siku 60 za mtoto wake huyo mwenye umri wa miaka 4 kwenye Chumba cha Wagonjwa Mahututi (ICU) katika Hospitali hiyo ya Rufaa ya Kanda ya Kati.

“watu walikuwa wanakuja, wanaruhusiwa wanamuacha mwanangu, wakati mwingine anabaki peke yake”. amesema Bi. Janeth.

Dkt. Venance Misago ni Bingwa wa Ganzi na Wagonjwa Mahututi, na Mkuu wa Idara ya Huduma za Uangalizi Maalumu BMH amesema, Moyo wa mtoto huyo ulisimama ghafla (cardiac arrest) mara nne (4) ndani ya siku 60 mtoto huyo alipokuwa ICU.

“aligundulika kuwa na maambukizi kwenye Ubongo (meningitis), hali iliyokuwa inasababisha apoteze fahamu mara kwa mara” alieleza Dkt. Misago.

Aidha, Dkt. Misago amesema kuwa kwa kawaida mgonjwa hukaa katika Chumba cha uangalizi maalumu siku 3 hadi 14 lakini maambukizi aliyokuwa nayo mtoto huyo yalisambaa kiasi cha kusababisha presha kushuka na kupelekea Moyo kusimama (septic shock) mara kwa mara.

Ingawa hali hiyo haikuwa rahisi kwa Bi. Janeth, hakusita kumshukuru Mungu, Madaktari na Wauguzi waliyomhudumia mwanaye.

“…nilipitia wakati mgumu kiasi cha kukata tamaa, namshukuru Mungu kwa kumponya mwanangu, nawashukuru Madaktari na wauguzi kwa kumpambania mwanangu” alieleza Bi. Janeth kwa furaha.

Kwa mujibu wa Awadhi Mohamed, Mkurugenzi Msaidizi huduma za Usitawi wa Jamii Hospitali ya Benjamin Mkapa imetumia Shilingi 10, 100,000 kugharamia dawa, vifaa tiba na chakula kwa kipindi chote cha siku 60 Mtoto wa Bi. Janeth alipokuwa ICU.

Kupona kwa mtoto huyo ni kielelezo cha faida za uwekezaji katika sekta ya Afya nchini, hasa mapinduzi yanayofanywa katika kuboresha huduma za Wagonjwa Mahututi.

Ingawa, wakosoaji wa serikali hasa Wizara ya Afya wamekuwa na jicho la kutoridhishwa na hatua za maboresho hususani kasi ya utekelezaji na ubora wa huduma, historia ni mwalimu mzuri.

Historia inakili kwamba, maboresho ya huduma ni mchakato, huduma za Afya nchini haziwezi kutokea ghafla mithili ya kimbunga, zinapitia mkondo huo huo wa mchakato wa maboresho ikiwa ni pamoja na huduma za ICU.

Mathalani, taarifa za Maktaba ya Historia ya Tiba ya Nchini Marekani zinadokeza mchakato wa maboresho ya huduma za ICU katika nchi za Ulaya ulianza kwa kanuni za kutenga majeruhi wa vita vya Crimean kwa kuwaweka mahututi jirani na vituo vya wauguzi (nursing stations) ili wapewe uangalizi maalumu.

Hiyo ilikuwa 1854, maboresho hayo yaliyohamasishwa na Bi. Florance Nightingale kusaidia kuokoa Maisha ya Majeruhi wengi wa vita, Ulaya ilisubiri karibu miaka 100 na mlipuko wa Polio kuwa na ICU ya kwanza, iliyojengwa 1953 huko Copenhagen, Denmark.

Hali hii ni tofauti na Tanzania, kwa mujibu wa Mheshimiwa Ummy Mwalimu (Mb), Waziri wa Afya, alipowasilisha Makadiliyo ya bajeti, mapato na matumizi ya Wizara ya Afya kwa mwaka wa Fedha 2023/2024, aliliambia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu hatua kubwa zilizopigwa katika huduma za Wagonjwa Mahututi.

Waziri huyo wa Sekta ya Afya, alinukuliwa Mei 12, 2023 akisema kuwa baada ya shambulio la Uviko 19, serikali imeweza kuongeza wodi za Wagonjwa Mahututi kutoka 45 had 258 ndani ya kipindi cha miaka 2, yaani 2020 hadi 2023.

“Tunaweza kulaza wagonjwa mahututi 1000 kila siku nchini” alisema Mhe. Ummy Mwalimu.

Hapana shaka, kama ilivyo kwa Mtoto wa Bi. Janeth, maboresho ya huduma za ICU yaliyofanyika katika kipindi hicho cha miaka 2 yamesaidia kuokoa maelfu ya Maisha ya Watoto na watu wazima waliyokumbwa na changamoto mbalimbali za kiafya zilizowalazimu kuhitaji ICU.

Mwaka 2020, Hospitali ya Benjamin Mkapa ilikuwa na Wodi ya Wagonjwa Mahututi yenye vitanda 6 pekee, lakini kupitia maboresho hayo, hadi Makala haya yanaandi.kwa, Hospitali hiyo ina Wodi mbili za wagonjwa Mahututi zenye vitanda 22.

Kwa mujibu wa Dkt. Misago, vitanda hivyo vina mashine za kusafisha mfumo wa hewa (Suction Machine), mashine za kusaidia kupumua (Ventilator), mashine za kusaidia Moyo, Figo na Kuzuia damu Kuganda (Syringe pump and Infusion Pump) pamoja na mashine za uangalizi wa mwenendo wa matibabu ya Mgonjwa (Monitors).

Hali hiyo, inasaidi kuokoa Maisha ya wanchi wengi wenye kuhitaji huduma hizo kwa uhakika, kumbuka iliichukua Ulaya miaka 99 kupata ICU ya kwanza, huku Tanzania ikijenga ICU zaidi ya 200 ndani ya siku 730.