April 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mtaturu aendesha harambee kuchangia ujenzi wa shule

Na Dotto Mwaibale, Singida

MBUNGE wa Singida Mashariki, Miraji Mtaturu ameendesha harambee ya ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Kijiji cha Matongo iliyopo Wilaya ya Ikungi mkoani Singida, ambapo zaidi ya sh. milioni 10 zilipatikana.

Mtaturu ambaye alikuwa mgeni rasmi katika harambee hiyo, ametoa mifuko ya saruji 100 kwa ajili ya kuanza kufyatua matofali ili ujenzi huo uanze mara moja.

Katika harambe hiyo, wananchi na wadau mbalimbali wa elimu wameshirikishwa ambapo licha ya kupatikana fedha hizo, pia ilipatikana mifuko ya saruji 259, maroli ya mchanga 15, bati bando mbili, matofali 1,000 na matela ya mchanga 10.

Fedha na michango hiyo inakwenda kuanza kujenga madarasa na kutatua adha ya wanafunzi wa kijiji hicho, ambao wanatembea umbali wa kilomita 13 kwenda kusoma Shule ya Sekondari ya Ikungi Mchanganyiko, jambo linalowasababishia kushindwa kuhudhuria vizuri masomo yao.

Akizungumza juzi katika harambee hiyo, Mtaturu amewaambia wananchi wa kijiji hicho kuwa elimu ndiyo mkombozi na kila mtu, anawajibu wa kuchangia ambapo aliwahakikishia kuwa serikali itaendelea kuboresha miundombinu ya shule na kutoa elimu bure bila malipo, kuanzia shule ya awali hadi kidato cha nne.

Amesema serikali itaendelea kujenga miundombinu ya elimu, kuongeza idadi ya walimu na kujali maslahi yao hivyo aliwaomba wafanye kazi kwa bidii kwani Rais, Samia Suluhu Hassan anawapenda watumishi wote hapa nchini.

Mtaturu ametumia nafasi hiyo kuwaeleza wananchi hao kuwa serikali, imepanga kuboresha miundombinu ya barabara katika jimbo hilo la Singida Mashariki ambapo nje ya bajeti yake ya mwaka huu, imetoa sh. bilioni 1.5 kwa kazi hiyo.

Akizungumzia sekta ya afya, amesema serikali katika bajeti yake ya mwaka huu imeongeza fedha ikilinganishwa na ya mwaka wa fedha uliopita.

Amesema serikali mbali ya kuboresha miundombinu ya barabara, itapeleka umeme na maji katika maeneo yote ya jimbo hilo kikiwemo kijiji hicho cha Matongo.

Katika hatua nyingine, Mtaturu amechangia mabati 200 kwa ajili ya kupaua madarasa mawili ya shule shikizi ya Kitongoji cha Mwau, ambayo yamejengwa kwa nguvu za wananchi.

Kukamilika kwa madarasa hayo, kutawapunguzia changamoto watoto wa eneo hilo kutembea umbali wa kilomita saba kila siku kwenda Matongo kwa ajili ya kupata elimu.

Akizungumza na wananchi wa Kitongoji cha Mbughantigha wakati akikagua ujenzi wa madarasa mawili yaliyojengwa kwa nguvu zao, amewataka wajenge madarasa mengine mawili na nyumba ya mwalimu ili shule hiyo iweze kupata usajili.

Mtaturu amesema, wametoka kwenye bajeti ya Serikali ya Awamu ya sita chini ya Rais, Samia ambayo imelenga kuwaletea wananchi maendeleo.

“Tunamshukuru sana rais kwa kuonesha upendo mkubwa kwa Watanzania tumuunge mkono,” amesema Mtaturu.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Ikungi, Abel Nkuwi amesema wanadhamira ya kujenga shule hiyo ya sekondari katika kijiji hicho, ili kuwasaidia watoto ambao wanatembea umbali mrefu kwenda Ikungi kupata elimu.

Amesema kwa utangulizi ujenzi wa shule hiyo, utagharimu sh. milioni 72 na kuwa wamepanga kila mwananchi mwenye uwezo katika eneo hilo, achangie sh. 15,000 ambapo wanatarajia kupata sh. milioni 48 hivyo kuanza mara moja kazi ya ujenzi, huku fedha nyingine zikitokana na harambee hiyo na vyanzo vingine.

Naye mwanafunzi, Nani Aley wa kidato cha pili anayetoka katika kijiji hicho kwenda kusoma Sekondari ya Ikungi Mchanganyiko, amesema kukamilika kwa ujenzi wa shule hiyo kutawaondolea changamoto ya kutembea kila siku kwenda shuleni na kuwapunguzia mzigo wa gharama wazazi wao kwa kuwapangia nyumba za kuishi wakiwa shuleni Ikungi.

Aley amemshukuru Rais, Samia kwa kuwapa elimu bure pasipo malipo pamoja na Mbunge wao Mtaturu, Diwani wa Kata hiyo na viongozi wote na wananchi kwa kuanza mchakato wa ujenzi wa sekondari katika kijiji hicho.