April 15, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mtandao mpya kuwafungulia Watanzania dunia mpya! Dola Milioni 100 zawekezwa

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

KATIKA juhudi za kukuza na kuimarisha mawasiliano ya kidijitali barani Afrika, Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (EIB Global) imetangaza kutoa ufadhili wa Dola za Marekani milioni 100 kwa kampuni ya mawasiliano ya AXIAN Telecom ili kusaidia upanuzi wa miundombinu ya mtandao wa simu katika nchi za Tanzania na Madagascar.

Ufadhili huo ni sehemu ya mkakati wa Global Gateway wa Umoja wa Ulaya, ambao unalenga kuwekeza katika maendeleo endelevu na ushirikiano wa kidijitali duniani, hususan katika nchi zinazoendelea.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa pamoja (Benki ya Umoja wa Ulaya, taasisi ya Global Gateway, pamoja na AXIAN Telecom) kusambazwa mapema leo imeeleza kuwa kupitia mradi huu, AXIAN Telecom inatarajia kupanua huduma za mtandao wa 4G katika maeneo mbalimbali ya Tanzania na Madagascar pamoja na kuendelea kusambaza huduma za mtandao wa kasi zaidi wa 5G.

Katika mgao wa fedha hizo, Tanzania imenufaika zaidi kwa kupokea Dola za Marekani milioni 60 huku Madagascar ikipokea Dola milioni 40. Huduma za AXIAN Telecom katika nchi hizi mbili zinapatikana kupitia chapa ya Yas.

Mkurugenzi Mtendaji wa AXIAN Telecom, Bw. Hassan Jaber alisema kuwa uwekezaji huo mkubwa utasaidia kwa kiasi kikubwa kuimarisha miundombinu ya mawasiliano ya simu na kufungua fursa mpya za kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa Tanzania na Madagascar.

“Ufadhili huu kutoka EIB Global utatuwezesha kupanua mtandao wa simu na huduma zake kwa watu wengi zaidi, na kuleta mabadiliko chanya katika jamii kupitia maendeleo ya kidijitali,” alisema Bw. Jaber.

Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa Benki ya Uwekezaji ya Ulaya, Bw. Ambroise Fayolle alisema, “Uunganishwaji wa kidijitali ni njia muhimu ya kufungua fursa katika elimu, biashara, afya na ujumuishaji wa kijamii. Mradi huu unaonyesha dhamira ya Benki ya Uwekezaji ya Ulaya ya kuwawezesha wananchi, kukuza maendeleo endelevu, na kuleta mabadiliko kupitia mawasiliano ya bei nafuu na ya kasi.”

Mradi huu unatarajiwa kupunguza changamoto ya upatikanaji wa huduma za mawasiliano katika maeneo ya vijijini na pembezoni mwa miji, hivyo kusaidia kupunguza tofauti za kijografia katika upatikanaji wa mawasiliano barani Afrika.

Kwa sasa, AXIAN Telecom inahudumia zaidi ya wateja milioni 44 katika nchi tisa za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, ikiwemo Tanzania, Madagascar, Senegal, Togo na Comoro.

Mradi huu mkubwa wa uwekezaji unatarajiwa kuwa chachu ya maendeleo ya uchumi wa kidijitali, kuongeza ujumuishaji wa kijamii na kuinua maisha ya watu wengi kupitia huduma bora na za uhakika za mawasiliano.