Na Daud Magesa, Timesmajira Online, Mwanza
MKURUGENZI wa Halmashauri ya Manispaaa ya Ilemela,Ummy Wayayu,amesema kuwa wameokoa kiasi cha milioni 26 kati ya bilioni 1.4 zilizopangwa kutekeleza ujenzi wa vyumba vya madarasa 44 ya shule za sekondari,matundu 72 ya vyoo,ukamilishaji wa maboma 15, ununuzi wa viti na meza 2,750.
Akitoa taarifa ya ujenzi wa miundombinu ya elimu wilayani humo kwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,Said Mtanda, Julai 12,2024 Wayayu amesema mwaka wa fedha 2023/24 waliidhinishiwa kiasi cha bilioni 2.4 za kujenga madarasa 80 kati ya hizo wamepokea bilioni 1.4.
“Miradi hiyo imekamilika kwa asilimia 100 kwa gharama ya bilioni 1.394 kati ya bilioni 1.4 na hivyo tumeokoa milioni 26 ambazo zimetumika kutengeneza viti 23 vya walimu,kukamilisha madarasa 4,ukarabati wa matundu 6 ya vyoo na ofisi mbili,ujenzi wa matundu mawili ya vyoo vya walimu na ujenzi wa ofisi ya walimu,”amesema Wayayu.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Said Mtanda ameipongeza Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela kwa kuokoa fedha hizo zilizotumika kufanya kazi nyingine.
“Kwa mjini ni nadra kufanya kazi chenchi ikabaki,miradi haiishi fedha zinaliwa halafu itakamilishwa kwa mapato ya ndani,kwa kitendo hiki Ilemela mmenifurahisha sana, msimamo wa serikali si lazima fedha zilizotengwa zitumike zote,tunaweza kuokoa zikafanya kazi nyingine,”amesema.
Mtanda amesema maeneo mengine fedha hizo zingeliwa ikabaki kazi ya kufikishana TAKUKURU,hivyo serikali imedhamiria kufanya mabadiliko katika sekta ya elimu pia kuboresha maslahi ya walimu ikiwemo kulipa madai ya malimbikizo yao.
“Walimu endeleeni kushirikiana na serikali na muwe wavumilivu mfanye kazi bila manung’uniko kwa sababu maendeleo yanapozidi changamoto zingine zinaibuka,bilioni 5.4 za maendeleo angalieni majengo yaliyojengwa na wananchi katika shule hii (Lumala) yakamilishwe kwa mapato ya ndani yafanane na mapya,”ameagiza Mkuu huyo wa Mkoa.
Naye Mbunge wa Jimbo la Ilemela,Dkt,Angeline Mabula,amesema changamoto ni mifumo kuchelewesha fedha kutolewa hivyo ameiomba serikali kuiboresha ili ifanye kazi haraka.
“Ilemela ya miaka 10 iliyopita haifanani na ya leo,bilioni 4.61 isingekuwa mdudu mfumo kazi ingeshafanyika pia bilioni 1.94 zimechelewa kutoka sababu ya mfumo, unachelewesha maendeleo,”amesema.
Awali Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Hassan Masala amesema miundombinu hiyo ya sekta ya elimu imechagizwa na Rais Dk.Samia,tangu aingie madarakani wananchi hawana habari ya michango ya maendeleo na kwa kumheshimu na kumshukuru si vema kukaa kimya.
More Stories
Madiwani Ilala watoa chakula kwa watoto yatima
Waziri Mkuu: Tumieni matokeo ya tafiti za kisayansi katika utekelezaji wa mipango ya kitaifa
Zaidi ya wananchi 32,000 Vijiji vya Wilaya za Morogoro na Mvomero kuanza kupata mawasiliano