January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mtakwimu Mkuu wa Serikali awataka watanzania kuhamasishana suala la sensa,kuacha kupotoshana kwa taarifa zisizo rasmi

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma.

MTAKWIMU Mkuu wa Serikali,Dkt.Albina Chuwa amekanusha taarifa ambazo amesema siyo rasmi zinazosambaa mitandaoni kuhusu  orodha ya majina ya makarani yenye kichwa cha habari”Orodha ya majina ya maombi ya kazi ya muda ya sensa ya watu na makazi yaliyohakikiwa na kujibiwa kikamilifu”.

Dkt.Chuwa amesema hayo jijini hapa leo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maombi ya kazi ya muda za sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022,ambapo amesema mchakato wa ajira za muda za makarani na wasimamizi wa sensa bado unaendelea katika ngazi ya kata/shehia na Halmashauri zote.

“Watanzania tuwe wazalendo,tuipende Nchi yetu tuache kupotosha umma badala yake tuhamasishane hili suala ni suala la kitaifa,

“Taarifa hiyo inayosambaa sio rasmi kwa watanzania waliyoomba nafasi ya ukarani na usimamizi wa sensa katika maeneo wanayoishi,kwenye taarifa inayofanana na hii ambayo pia siyo rasmi,watu hawa ambao hawana nia nzuri kwa serikali na watanzania kwa ujumla wamekwenda mbali na kutamka tarehe ya usahili kuwa ni Mei 29 mwaka 2022 jambo ambalo siyo kweli,”amesema Dkt.Chuwa.

Amesema zoezi la uchambuzi wa maombi kwa waombaji wote linatarajiwa kuanza Juni 2 mwaka huu kwenye kila Kata au Shehia husika baada ya kukamilika kwa mafunzo ya maafisa watakaohusika kufanya usaili huku akisema mchakato wa ajira za kuwapata makarani na wasimamizi wa sensa linakwenda vizuri kulingana na ratiba ya sensa.

Mei 5 mwaka huu serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilitangaza rasmi kuanza kupokea maombi ya kazi za muda za makarani na wasimamizi wa sensa ya watu na makazi itakayofanyika  Agosti 23 mwaka huu kupitia mfumo wa maombi wa kielektoniki ambapo hadi kufikia tamati ya maombi waombaji 689,935 walifanikiwa kuomba kati ya 205,000 wanaohitajika kwenye zoezi la sensa ya watu na makazi.