Na Mwandishi Wetu,Dodoma
MKUU wa Kitengo cha Huduma za Uzazi wa Mpango hospitali ya Makole jijini Dodoma Loy Mazengo amewaasa wadau wa masuala ya afya ya uzazi kuifanya elimu ya huduma za uzazi wa mpango kuwa endelevu hususan kwa vijana ili waweze kupata elimu sahihi ya matumizi ya huduma hizo bila kuathiri matarajio yao.
Akizungumza na mtandao huu Mazengo ambaye kwa taaluma ni Muuguzi amesema,elimu hiyo itawasaidia kuondoa unyanyapaa kwa vijana na hivyo kwa wale ambao wameshaingia kwenye mahusiano kuwa na elimu sahihi ya kujikinga na mimba zisizotarajiwa lakini pia kufikia malengo yao hasa ya kimasomo.
“Kijana akija ni lazima apate huduma kwa sababu ,mpaka amefika kwako tayari ameshajiingiza katika mahusiano kwa hiyo utakapoacha kumpa huduma utamtafutia matatizo mengine wakati bado hajatimiza ndoto zake ,anatakiwa asome amalize kuliko kukosa huduma itakayomsababishia kupata ujauzito akakatisha masomo yake na hivyo kushindwa kufikia malengo yake.” Amesema Loy na uongeza kuwa
“Jamii bado haina elimu ya kutosha kuhusu matumizi ya huduma za uzazi wa mpango kwa vijana ,wapo wanaodhani kama tunawahamasisha kufanya vitendo vya ngono lakini siyo kweli ,hii ni kwa sababu tayari wao wenyewe wanakuwa wameshaingia kwenye mahusiano hivyo ni vyema wapate huduma zitakazowakinga kupata mimba zisizotarajiwa lakini pia kupewa elimu sahihi ya matumizi ya nia za uzazi wa mpango kulingana na umri wao.”
Aidha amesema kama kijana hatapata elimu sahihi ya matumizi ya njia ipi inamfaa kwa umri wake anaweza kujiingiza kwenye njia zisizo sahihi kama vile sindano na hivyo kumsababishia matatizo pindi atakapohitaji kupata mtoto hapo baadaye.
“Njia hii ya sindano huwa hatushauri itumike kwa mtu yeyote ambaye hajawahi kuzaa au aliyezaa mtoto mmoja kwa sababu inaweza kumletea shida ya kuchelewa kupata mtoto pindi atakapohitaji,hivyo ni vyema jamii ipate elimu ya kutosha kuhusu umuhimu wa matumizi ya huduma za uzazi wa mpango wa vijana kwa maslahi yao binafsi na Taifa kwa ujumla “
Ester Amos na Justine Joseph ni wanafunzi wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) nao wamesema,upo umuhimu wa kuhakikisha kila kijana ambaye ameshaingia katika mahusiano ,anapata elimu sahihi ya matumizi ya njia za uzazi wa mpangoj na afya ya uzazi kwa ujumla.
Aidha Mratibu wa Uzazi wa Mpango Taifa Zuhura Mbuguni akizungumza wakati wa mafunzo kwa waandishi wa habari kuhusu masuala ya huduma za uzazi wa mpango amesema kama kijana amejitambua katika matumizi ya uzazi wa mpango itamwezesha kufikia matarajio yake hasa ya kumaliza masomo yake.
“Drop out nyingi hasa kwa wasichana katika shule za msingi na sekondari zinatokana na mimba za utotoni lakini kama kijana amejitambua katika matumizi ya uzazi wa mpango itamwezesha kufikia matarajio yake hasa ya kumaliza masomo yake.”amesisitiza Zuhura
More Stories
AZAKI yawasilisha mapendekezo yao kwa Serikali katika kuboresha Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050
CP.Wakilyamba :Uvamizi maeneo ya hifadhi ya taifa katavi haukubaliki
Watu wawili wanaodhaniwa majambazi wapigwa risasi na Polisi