Na Joyce Kasiki, TimesMajira Online, Chamwino
WAZAZI na walezi wameshauriwa kuwajengea watoto misingi mizuri tangu wakiwa na umri wa kuanzia miaka 0-8 kwa kuwa kipindi hicho, ndicho mtoto anaelewa mambo kwa haraka.
Hayo yamesemwa na Mkufunzi wa Shirika la Kusaidia Watoto wanaopitia Changamoto mbalimbali (CiC) Frank Samson, wakati akitoa mada kwa walimu wa madarasa ya awali wilayani Chamwino mkoani Dodoma kuhusu makuzi ya awali kwa binadamu.
Amesema katika kipindi hicho ndio wazazi na walezi wanaweza kufundisha watoto mambo mema au mabaya kutegemeana na mazingira wanayoishi na baada ya hapo fursa ya kumjenga mtoto katika mambo mbalimbali inazidi kupungua.
Mkufunzi huyo amesema katika kipindi hicho mtoto anajengwa vizuri katika lugha, hisia, kiakili, kimwili, kiutamaduni na kujongea.
“Katika umri wa miaka 0-8 ndio misingi ya mwanadamu unajengwa,akivuka umri huo fursa ya kumjenga katika mambo mbalimbali inazidi kupungua,” amesema Frank na kuongeza;
“Lakini katika umri huo ndio mtoto anaweza kujifunza mambo mabaya, unakuta wazazi wanagombana, wanatukanana matusi kila siku, ni lazima mtoto huyu atajifunza kutukana.”
Lakini pia Frank amesema,mtoto katika umri huo hujifunza kupitia milango mitano ya fahamu ambayo ni pua(kunusa),sikio (kusikia),mkono (kugusa),jicho (kuona) na ulimi (kuonja).
More Stories
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa
NLD kipo tayari kwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa