Na Mwandishi wetu, Timesmajira online
MKUU wa Chuo cha Veta Furahika Dkt David Msuya ameipongeza Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kufadhili wanafunzi 200 waliotoka katika kaya masikini kusoma katika chuo hicho.
Dkt Msuya ametoa pongezi hizo Jijini Dar es salaam mapema leo Novemba 11,2024 wakati akizungumza na waandishi wa habari amesema wamepokea wanafunzi hao kutoka Zanzibar kwa ajili ya kusoma kozi mbalimbali ikiwemo ushonaji na mapambo.
“Namshukuru Rais Dkt Hussein Alli Mwinyi na Serikali yake kwa ujumla kwa kuthamini vijana waliotoka katika mazingira magumu na kuona umuhimu wa kuwaendeleza kielimu ili waweze kujikwamua kimaisha na kuwaondoa kwenye vishawishi”, amesema Dkt Msuya.
Amesema mafunzo hayo yanatolewa bure katika chuo hicho lengo likiwa kuhakikisha vijana wanatumia fursa hiyo kupata ujuzi ili waweze kujikwamua na kujiepusha vishawishi mitaani.
Aidha Dkt Msuya amempongeza Mkurugenzi wa maendeleo ya jamii Zanzibar kwa kuonyesha ushirikiano na chuo hicho ili kuhakikisha vijana wanapata ujuzi na kujitegemea.
Pia, ametoa wito wa wazazi na walezi kupeleka watoto wao katika chuo hicho kwani mafunzo ni bure na dirisha la usajili lipo wazi.
“Niwaombe wazazi na walezi pasipo kujali itikadi ya dini wala siasa wawalete watoto wapate ujuzi hapa elimu ni bure na tunakozi nyingi ambazo mtoto akitoka hapa ataweza kujiajili na kuajilika”,amesema
Katika hatua nyingine Dkt Msuya amesema Chuo hicho kimeongeza kozi ya Tehama lakini pia wanatarajia kuanzisha kozi ya ufundi wa pikipiki ili kuhakikisha wanamgusa kila kijana ili waweze kujitegemea.
Kwa upande wake Mwanafunzi Safia Hamis Mwinyi ameishukuru Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kuwafadhiri na anaamini elimu hiyo itaenda kuwasaidia kujikwamua kiuchumi na kuwaondoa kwenye utegemezi na kuweza kuwasaidia wazazi wao.
More Stories
Wapinzani kutimkia CCM ishara ya ushindi Uchaguzi Serikali za Mitaa
Vikundi Ileje vyakabidhiwa mikopo ya asilimia 10, DC Mgomi avipa somo
Wananchi Tandale wahimizwa kuchagua viongozi sahihi