Na Yusuph Mussa, Timesmajira Online,Handeni
MBUNGE wa Jimbo la Handeni Vijijini mkoani Tanga John Sallu amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia gari la kubeba wagonjwa (Ambulance), na wao kwa umuhimu wake, wameamua kulipeleka Kituo cha Afya Msomera.
Akizungumza kwenye hafla fupi ya kukabidhi gari hilo iliyofanyika kijiji cha Msomera, Sallu amesema wameamua kupeleka gari hilo Kijiji cha Msomera ili kuwajali wananchi waliopo na wale wanaoongezeka kuhama kwa hiari kutoka Hifadhi ya Ngorongoro (NCA) mkoani Arusha.
Sallu amesema wataendelea kuboresha huduma za kijamii kwenye kijiji hicho ambapo ukiacha huduma za afya kwa kuwepo zahanati ya Msomera na Kituo cha Afya Msomera pia kijiji hicho kina maji, umeme, barabara na mawasiliano ya simu.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Mussa Mwanyumbu amesema gari hilo limeletwa kwa ajili ya rufaa kutoka Kituo cha Afya Msomera kwenda hospitali kubwa, hivyo anaamini litakuwa msaada mkubwa kwa wananchi wa kijiji hicho.
Mkuu wa Wilaya ya Handeni Wakili Albert Msando alimshukuru Mbunge wa Handeni, Sallu kwa kupendekeza gari hilo lipelekwe Kituo cha Afya Msomera, kwani mahitaji ya ambulance kwenye Wilaya hiyo ni makubwa angeweza kupeleka sehemu nyingine.
Akisoma taarifa kwa niaba ya Kaimu Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Dkt. Kisaka Godfrey, Katibu wa Afya wa Halmashauri hiyo Upendo Mkala amesema halmashauri hiyo ilipokea kiasi cha milioni 650 kutoka Serikali Kuu na milioni 50 kutoka mapato ya ndani ya halmashauri kuanzia 2021 hadi 2024 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya afya.
“Fedha hizi ilikuwa kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Msomera (majengo), ukarabati wa Zahanati ya Msomera na ujenzi wa Zahanati ya Mkababu pamoja milioni 450 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba kwa vituo vipya vya afya ikiwemo Msomera na Sindeni” amesema Mkala.
Mkala amesema moja ya changamoto kwenye Kituo cha Afya Msomera ni wodi ya wanaume,wanawake na jengo la kuhifadhia maiti.
Pia uhaba wa watumishi, ukosefu wa nyumba za watumishi kwa kuwa fedha zilizopokelewa hazikukidhi ujenzi wa nyumba hiyo.
“Mikakati yetu ni kutenga bajeti na kuomba kibali cha kuajiri watumishi pamojana fedha kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya majengo yaliyobaki hasa majengo ya wodi, jengo la kuhifadhia maiti na nyumba za watumishi kutoka Ofisi ya Rais- TAMISEMI,”amesema na kuongeza
“Sanjari na kutenga bajeti na kutafuta wahisani kwa ajili ya kujenga visima vya kuvuna maji ya mvua,”.
More Stories
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa
NLD kipo tayari kwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa