March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Msita :Nimeona dhamira ya dhati ya Rais Samia

Na Joyce Kasiki,Dodoma

Mbunge wa Jimbo la Itigi Yohana Msita ameunga mkono hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyotoa wakati wa uzinduzi wa Bunge la 13, akisema ameona dhamira ya dhati ya Rais ya kuipeleka nchi katika mwelekeo sahihi wa maendeleo.
Akichangia hotuba hiyo bungeni, Mbunge huyo amesema Rais amegusa kwa kina masuala ya utumishi wa umma na utawala bora kwa kuzingatia ukweli na uwazi, akisisitiza kuwa kama taifa litasimama katika misingi ya uwajibikaji na uwazi, Tanzania itapiga hatua kubwa za kimaendeleo.
“Watanzania tuna imani kubwa na Rais wetu kwa hatua anazoendelea kuchukua. Ndani ya kipindi cha miaka mitano ijayo, tunaamini tutafika pale tunapotamani kuona taifa letu likifikia,” amesema Mbunge huyo.
Katika suala la usimamizi wa fedha na rasilimali, Mbunge wa Itigi amesema jimbo lake limekuwa miongoni mwa wanufaika wakubwa ndani ya miaka minne iliyopita kutokana na usimamizi mzuri wa mali za umma. Ameeleza kuwa hospitali ya kisasa yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 1.75 imejengwa, pamoja na ujenzi wa barabara zenye urefu wa kilomita 10 katika jimbo hilo.
Aidha, Mbunge huyo ametaja matarajio makubwa ya wananchi wa Itigi kunufaika na mradi wa treni ya mwendo kasi, ambapo kituo kikubwa kinatarajiwa kujengwa katika eneo hilo, akisema utekelezaji wa miradi hiyo ni ushahidi wa moja kwa moja wa usimamizi bora wa fedha za umma.
Kuhusu Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Mbunge huyo amesema ana matumaini kuwa taasisi hiyo itafanya kazi kwa ufanisi zaidi ndani ya miaka mitano ijayo, huku Bunge likiwa tayari kushirikiana nayo katika mapambano dhidi ya rushwa ili kuhakikisha mafisadi wanawajibishwa.
Akiunga mkono hoja iliyotolewa awali na Mbunge wa Kangi Lugola, Mbunge wa Itigi amesema kuna haja ya kujenga shule maalum za michezo katika kila kanda nchini ili kuchuja na kukuza vipaji vya michezo na hatimaye kupata wachezaji bora watakaolitangaza taifa.
Katika mchango wake kuhusu utamaduni, Mbunge huyo amesema sekta hiyo haijapewa kipaumbele cha kutosha, akieleza kuwa mjadala mwingi umejikita zaidi kwenye lugha ya Kiswahili pekee. Amesema Tanzania ina utajiri mkubwa wa kiutamaduni ambao bado haujatumiwa ipasavyo.
“Mojawapo ya mambo tungetamani kuyaona ni Tanzania kuwa na vazi rasmi la taifa. Tumeona katika mashindano ya kimataifa kama AFCON, mataifa mengine wanaposhuka wanatambulika moja kwa moja. Sisi Watanzania ni lini tutakuwa na vazi letu rasmi ili popote tunapokwenda tujulikane?” amehoji.
Amesisitiza kuwa usimamizi mzuri wa fedha, utawala bora, kukuza michezo na kulinda utamaduni ni nguzo muhimu za maendeleo ya Taifa.
Kama ungependa: