December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Msingi wa HDT kutaka taasisi za fedha kimataifa kusamehe madeni

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira,Online Dar

KUANZIA wiki ijayo Benki ya Duniani (WB) inaanza vikao vyake vya mwaka kwa ajili ya kujadili masuala mbalimbali yanayohusu benki hiyo.

Benki hiyo inaanza vikao vyake huku kukiwa na ombi la Rais John Magufuli alilolitoa Aprili 22, mwaka huu wakati akizungumza na wakuu wa vyombo vya Ulinzi na Usalama akiwa Chato, mkoani Geita kuhusiana na ugonjwa wa Corona.

Pamoja na mambo mengine, Rais Magufuli aliziomba zote za Afrika kuungana kuziomba taasisi za kifedha za kimataifa ikiwemo Benki ya Dunia ambazo zilitangaza kusaidia Mataifa ya Afrika (dhidi ya mapambano ya Corona), kutoa msamaha wa madeni badala ya kutaka kukopesha mikopo mingine ilihali nchi hizo zinakabiliwa na madeni ya mikopo ya zamani.

Wiki hii Shirika la Health Promotion Tanzania (HDT), limeunga mkono wito wa Rais Magufuli, kuziomba taasisi za fedha kimataifa ikiwemo Benki ya Dunia (WB), ambazo zilitangaza kusaidia Mataifa ya Afrika, kutoa msamaha wa madeni hayo badala ya kutaka kukopesha mikopo mingine wakati zinakabiliwa na madeni ya mikopo ya nyuma.

Mkurugenzi wa HDT, Dkt. Peter Bujari alitangaza uamuzi wa shirika hilo kuunga mkono kauli ya Rais Magufuli, wiki iliyopita jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kampeni ya Msamehe wa Deni la Afya (DR4H).

Dkt. Bujari anasema; “Haya tunayoyafanya sasa hivi hayahusiani na kampeni zinazoendelea (za uchaguzi mkuu) isipokuwa sisi tunafanyakazi zetu za kitaalam tukijua mwezi huu, wiki ijayo (wiki hii) kuna mikutano ya mwaka ya Benki ya Dunia ambayo inaanza Marekani.

Kwa hiyo kabla hawajaanza mikutano hiyo tumeona ni vema tupaze sauti zetu ili kuwaambia nchi zetu zimekopa, lakini hali ya makusanyo itakuwa ndogo kwa sababu ya Covid-19, kwa hivyo badala ya kutukopesha pesa zingine, basi yale madeni tuliyokopa zamani ama yasogezwe mbele ama yasamehewe au yasiwe na riba.”

Anafafanua kwamba ikiwa nchini yetu itakopeshwa tena mzigo wa madeni utazidi kuwa mkubwa zaidi, ndiyo maana wameona huu ni wakati muafaka na kutoa wito kwa taasisi hizo kusamehe madeni hayo badala ya kutukopesha tena.

Akitaja sababu nyingine ya kuomba msamaha huo, Dkt. Bujari anasema Aprili, mwaka huu wakati hali ya Covid-19 ilivykuwa tete nchini, Serikali iliamua kutenga vituo vya wagonjwa hao ikiwemo Hospitali ya Amana na Mloganzila, lakini kulikuwa na changamoto nyingi za utoaji huduma kwa wagonjwa.

Mkurugenzi wa Shirika la Health Promotion Tanzania (HDT), Dkt. Peter Bujari (kulia) akisisitiza jambo.

Anaema wanashauri taasisi hizo zikikubali kutoa msamaha huo fedha hizo,ili zikija zielekezwe kuboresha miundombinu ya afya ili kikidhi mahitaji ya kukabiliana na magonjwa ya milipuko yanayoweza kutokea hapo baadaye.

Anatoa mfano kwamba mwaka 2012/13 mikopo ambayo Serikali ilikopa kutoka maeneo mbalimbali ilikuwa ni sh. trilioni 5.01. “Mwaka 2021/21 pesa ambayo Serikali imekopa ni sh. trilioni 10.6, kwa hiyo nchi yetu inakopa kama zilivyo nchini zote duniani,” anasema na kuongeza;

“Ukikopa inakupasa ulipe na kila mwaka Serikali yetu inatega bajeti ya kulipa mikopo ile.

***Takwimu za IMF

Dkt. Bujari anasema wanaongea habari za kutaka kusamehewa madeni hayo kwa sababu kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na IMF Juni, mwaka huu inakadiria kwamba ukuaji wa uchumi wa Tanzania utashuka kutoka asilimia 6.9 hadi asilimia 2.5 kwa sababu mbalimbali.

Moja ya sababu hizo zilizoanishwa na IMF kwa mujibu wa Dkt. Bujari kuathirika kwa vyanzo vya fedha kutokana na Covid-19 iliyoathiri mataifa yote duniani.

“Mfano, moja ya vyanzo vyetu vya pesa ni utalii. Sasa baada ya nchi nyingi kufunga mipaka yake watalii hawaji, kwa hiyo mapato tuliyotegemea kuyapata maeneo hayo yamepungua au yatakuwa ni kidogo sana,” anasema.

Anazidi kufafanua kwamba kwa jumla maksio ya mapato yetu kama nchi yatapungua na hii sio Tanzania peke yake, bali hata nchi nyingine na kuna nyingine duniani uchumi wake utashuka pungufu ya 0.

“Kwa hiyo sisi tuna nafuu kidogo uchumi wetu unategemea kupungua kutoka asilimia 6.9 hadi 2.5 (kwa mujibu wa IMF).”

Hata hivyo anasema pamoja na athari hizo wale wanaotudai, bado wanaendelea kutudai, wakitaka walipwe deni lao kwa sababu tulishakopa zamani.

“Wanatudai wakati kwa upande mmoja makusanyo yetu kama nchi yamepungua maana yake tuna pesa kidogo za kutumia, lakini kwa upande wa pili wale waliotukopisha wanataka tuwalipe pia,” anasema Dkt. Bujari na kuongeza;

“Ikiwa tutawalipa wale waliotukopesha kama vile ambavyo tulikusudia, maana yake tutakuwa hatuna pesa ya kuendesha mambo ya muhimu kama nchi.”

Mtaalam wa afya

***Mlipuko wa Covid-19

Anazidi kufafanua kwamba Covid-19 ilivyokuja Machi na Aprili, mwaka huu hali ilikuwa ni tete kwa sababu mfumo wa afya haukuwa umejiandaa kikamilifu kukabiliana na hali ya hali hiyo.

Anasema vituo vilivyotengwa kwa ajili ya kulaza wagonjwa vilizidiwa na huduma zilishuka, lakini pili miundombinu ya vifaa vya kusaidia wagonjwa kupumua haikuwa mizuri.

“Je tulikuwa na Oxygen za kutosha kwa ajili ya kuwasaidia wagonjwa hao wote kupumua? Maana kama una wagonjwa 100 basi uwe na mitungi 100 ya kuwawekea wagonjwa wale kuwasaidia kupumua,” anasema na kuongeza;

“Tulijikuta mifumo yetu ya afya ikiwa imetengenezwa sio kwa ajili ya kushughulikia watu wengi kiasi hicho na huu mlipuko pengine sio wa mwisho, pengine kuna mwingine utatokea baadaye.”

***Ni nini hoja ya HDT

Kwa mujibu wa Dkt. Buhari hoja yao sasa kama wadau wa afya ni kuwa huu sasa ni wakati wa kujipanga kama nchi kuboresha miundombinu ya afya na mifumo mingine ili litakapotokea janga jingine, basi mifumo yetu ya afya iweze kuwasaidia Watanzania.

Anafafanua kuwa mambo mengine yote yanayofanywa na Serikali ni ya muhimu, lakini janga likitokea kila mtu anakimbilia kituo cha afya, zahanati iliyo karibu na kwenye hospitali ili kupata matibabu.

“Janga likitokea, duniani mipaka inafungwa, kwa hiyo hauwezi kusema utakimbizwa Nairobi, Afrika Kusini na kwingineko kupata matibabu, kwa sababu nako watakuwa wamefunga mipaka ndege haziendi na hata mipaka ya vichochoroni nayo imezuiwa,” anasema na kusisitiza;

“Kwa hiyo sisi tunafikiri kuwa tukipata msamaha wa madeni kama tunavyo dai au wakaahirisha muda wa kulipwa ni wakati muafaka wa sisi kama nchi tukatumia fedha hizo kuboresha mfumo wa afya ili ikitokea dharura yoyote baadaye mifumo yetu iweze kutusaidia Watanzania kupata matibabu sitahiki.”

Anasema mwaka huu wa fedha 2020/2021 bajeti iliyopitishwa kwa mujibu wa Waziri wa Fedha ni Trilioni 34.878, ambapo kwenye bajeti hiyo imepanga bajeti ya kulipa madeni sh. trilioni 10.4 sawa na asilimia 29.9.

“Kwa hiyo karibu asilimia 30 tunaitumia kulipa madeni tulilokopa nje, wakati mapato yetu ya ndani ambayo tunayakusanya ni sh. trilioni 24.07 sawa na asilimia 69 ya bajeti yetu.

Kwa msingi huo fedha zinazokopwa nje ni karibu zinalingana na zile ambazo tunalipa madeni. Sasa swali ni kwamba ikiwa mapato yanatarajia kupungua maana yake ni kwamba pesa ambazo Serikali itazikusanya ndani ya nchi zitakuwa pungufu ya trilioni 24.07.

Ikiwa fedha tunazokusanya zitapungua na ikiwa tutalipa deni kama tulivyopanga kulipa, basi maana yake ni kwamba pesa tulizonazo kwa ajili ya matumizi ya nchi uwezo huo utapungua,” anasema na kuongeza;

“Mazingira haya sio kosa la Tanzania, sio kosa la Serikali ni shida imetokea dunia nzima ambayo imegusa mataifa hiyo. Ndiyo maana tunasema kwamba kwa vile ili janga ni la dunia nzima, huu sio wakati wa wafanyabiashara (taasisi za fedha za kimataifa) kupata faida kubwa , bali ni wakati wa wafanyabiashara waliotukopesha kufikiria namna ya kusaidia hizi nchi.”

***Kwa nini wanapaza sauti

Kwa mujibu wa Dkt. Bujari wanaamini wakipaza sauti zao zitasikika na taasisi hizo zitaahirisha muda wa kulipwa madeni, kupunguza riba au kusamehe kabisa na hayo yakifanyika basi sehemu kubwa ya fedha hizo Serikali izielekeze kuboresha miundombinu ya afya.

Alisema baada ya Covid-19 kuingia ilikuwa taasisi za fedha duniani zikopeshe nchi zinazoendelea ili kuziongezea kwa ajili ya kukabiliana na changamoto hiyo na kwamba maana yakehilo lilikuwa ni deni lingine tena.

***Huu sio wakati wa kuongeza deni

Dkt. Bujari anasema wao (HDT) wanafikiri kwamba huu sio wakati wa kuongeza deni, bali ni wakati wa kusaidiana. “Kwa hiyo taasisi hizo zina njia mbili, kuahirisha madeni, au kufuta riba au kutusamehe madeni.”

“Tunashauri wale waliokopesha Serikali, badala ya kukopesha tena wafikirie kutusamehe madeni au riba ili Serikali zetu ziweze kuwa na pesa kwa ajili kuboresha mifumo ya afya na kusaidia watu ambao wamepata changamoto.”

***Pongezi

Anapongeza juhudi ambazo zimeishafanyika katika hilo akitolea mfano IMF akisema Juni mwaka huu walipitisha fedha kwa ajili ya kuipa Tanzania, akimnukuu waziri wa fedha.

“Tunaamini hicho ni kitu kizuri na tunafiriki taasisi zingine zitafanya hivyo,” anasema na kuongeza kwamba WB nao wamesema inawezekana wakatoa pesa kwa ajili ya kusaidia Tanzania kwenye mfuko wao unaotoa unafuu wa kiuchumi, kiafya na mambo ya kijamii.

***Wazilima barua

Dkt. Bujari anasema tayari wameziandikia barua taasisi za fedha duniani pamoja na barua pepe ili WB wanapoanza mkutano wao ujumbe uwe umewafikia kuwa sauti kutoka Tanzania zinasema hayo.

***Wito

Anasema wito wao ni kwamba huu sio wakati wa kukopeshana, kwani mtu akikopa wakati uwezo wake wa kukusanya pesa ndani umepungua sana maana yake hataweza kulipa.

Anatoa mfano kuwa katika Afrika kuna nchi tano uwezo wake wa kukopa umefikia mwisho na zimewekwa kwenye mstari mweusi tayari kwamba haziweze kukopa kwa sababu madeni yamekuwa makubwa sana.

Alisema Tanzania haitaki kufika huko ndiyo maana wanataka nchi na taasisi ambazo zimesaidia nchi zipunguze madeni au zisamehe madeni.

. Bujari akisisitiza jambo

***Wito kwa Serikali

Dkt. Bujari anasema wanashauri pesa itakayopatikana kutoka kwenye msamaha wa madeni, Serikali ielekeze kiasi kikubwa cha fedha hizo sekta ya afya kwa sababu kila mmoja wetu nchini likitokea janga anakimbilia hospitali.

Anasisitiza kwamba uwezo wetu kwa sasa wa kukabiliana na milipuko, kuhudumia wagonjwa wanaumwa sana kwa pamoja upo chini, kwani baadhi ya hospitali za wilaya hazina Chumba vya Uangalizi Maalum wa Wagonjwa (ICU), lakini kama kipo ni kidogo chenye vitatu vitatu.

“Sasa je watakapokuwa ni wagonjwa 10 tutafanyaje? Kwa hiyo uwezo wetu wa kuwasaidia wagonjwa kupumua, uwezo wetu wa kuwapa wahudumu wetu wa afya ukoje wakati sisi tutakapokuwa tumejificha majumbani, lakini uwezo wa kuwapa vifaa vya kuwakinga bado uko chini,”alisema.

Alifafanua kwamba wanahitaji kutengeneza mifumo ya afya kwa kununua vifaa vinavyohitajika ili ikitokea dharura tuwe na kiwanda cha kutengeneza vifaa, lakini kuwe na vifaa ambavyo vimetengenezwa kwa ajili ya kusaidia watumishi wa afya