October 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Msimu wa nne,tuzo za eagle entertainment, kufanyika kivingine

Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza

Msimu wa nne wa tuzo za Eagle Entertainment kufanyika kwa Kanda ya Ziwa,ifikapo Desemba 14,2024, huku tuzo 28, zitatolewa kwa washindi mbalimbali ikiwemo, waandishi wa habari,wasanii, wajasiriamali na wengine.

Mashindano hayo kwa mara ya kwanza yalifanyika mwaka 2021 kwa ngazi ya Wilaya ya Sengerema,mwaka 2023 yaliofanyika kwa ngazi ya Mkoa wa Mwanza,na mwaka huu yatafanyika kwa ngazi ya Kanda ya Ziwa,lengo ni kutambua na kuwaongezea thamani,wahusika wa sekta mbalimbali,ambao wamekuwa na mchango katika maendeleo ya Taifa.

Akizungumza Oktoba 2,2024,na waandishi wa habari mkoani Mwanza, Mkurugenzi wa taasisi ya Eagle Entertainment, Hassan Kuku,wakati akitambulisha tuzo hizo kwa ngazi ya Kanda ya Ziwa pamoja na ufunguzi wa pazia la kuwapata washiriki watakao shindana kuwania tuzo hizo.

Ameeleza kuwa,kila siku wanazidi kupanua wigo katika tuzo hizo,ambapo mwaka 2021 walioanza na tuzo 12, mwaka 2023 tuzo 22 na mwaka huu wanatarajiwa kutoa tuzo 28.Pia wanatarajia kumualika Naibu Waziri Mkuu Doto Biteko,kuwa mgeni rasmi.

Pia ameeleza kuwa,tuzo hizo zipo tofauti na nyingine, kwani zinashirikisha kada tofauti kwa wakati mmoja ikiwemo wasanii, wajasiriamali, waandishi wa habari,mpiga picha na wengine.

“Tuzo hizi zitatolewa wilayani Sengerema mkoani Mwanza.Pazia la washiriki kutuma kazi zao, limefunguliwa Oktoba 2,2024,litafungwa Oktoba 23,2024.Tumepiga hatua tangu tulipo anza mapaka sasa,nawaomba wadau na taasisi mbalimbali,kutuunga mkono ili kufanya tuzo hizi kuwa bora zaidi,”ameeleza Kuku.

Meneja Uhamasishaji na Burudani wa Tuzo hizo,Albert Sengo,ametaja vipengele vitakavyo shindaniwa ni pamoja na msanii bora wa kike kwa mwaka 2024, msanii bora wa kiume,wimbo bora muongozaji bora wa video za muziki ,mpiga picha bora,tamasha bora la mziki,mshehereshaji bora,Dj bora,mtangazaji bora,filamu bora.

“Mwandishi bora wa habari za mazingira,hii itakuwa katika kuhamasisha utunzaji wa mazingira,tuzo ya uandishi wa habari bora wa kupinga vitendo vya ukatili,uandishi wa habari bora za elimu,msanii bora chipukizi,msanii bora wa hip hop,kundi bora la wajasiriamali,muigizaji bora na wengine.Tuzo hizi zinawahusu watu wa Kanda ya Ziwa tu,”ameeleza Sengo.

Naye Mratibu wa Tuzo hizo Oscar Zacharia, ameeleza kuwa,kuwapta waandishi wa habari bora katika vipengele vya mazingira, ukatili na elimu,majaji watakuwa wahariri wa vyombo vya habari,huku ya kikundi cha wajasiriamali bora jaji atakuwa Ofisa Maendeleo ya Jamii kutoka Wilaya ya Sengerema au Mkoa wa Mwanza.Huku wasanii,watapigiwa kura na wananchi kupitia web site ya www.eagleentertainmentaward.co.tz.

Mmoja wa waandishi wa habari mkoani Mwanza,Sarah Onesmo-,amewahimiza waandishi hususani wa kike kutumia fursa hiyo kutuma kazi zao ili ziweze kushindanishwa,hali itakayo chochea utendaji wa kazi.

Msanii H-Baba amewaomba wadhamini kuwaunga mkono katika tuzo hizo,ili kunyanyua watu wa Kanda ya Ziwa huku akiwahimiza wasanii kutuma kazi zao kwa wingi.