December 27, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Msimu shindano la Stories of Change wazinduliwa

Na Jackline Martin, TimesMajira Online

BAADA ya mafanikio ya Shindano la Uandishi la “Stories of Change” katika Mwaka 2021, 2022 na 2023, kwa mara nyingine, JamiiForums imezindua msimu mpya wa Shindano hilo kwa Mwaka 2024 kwa kushirikiana na Taasisi ya TWAWEZA.

Akifungua msimu mpya wa shindano hilo mwishoni mwa wiki,  Mkurugenzi Mtendaji wa JamiiForums, Maxence Melo, alisema dhima ya Shindano la ‘Stories of Change’ (SoC) Mwaka 2024 ni “Tanzania Tuitakayo” ikilenga kuhamasisha wananchi kuibua mawazo mbadala ya nini kifanyike kuipata Tanzania iliyo bora zaidi kwa kupendekeza mawazo bunifu.

Alifafanua kuwa mawazo hayo ni lazima yawe yale yanayoweza kutekelezeka ndani ya miaka mitano hadi 25 ijayo na kuwa sh. Milioni 50 zimetengwa kwa ajili ya washindi watakaoshiriki katika shindano hilo linalotarajiwa kuanza Mei Mosi, 2024 hadi Juni 30, 2024.

“Kwa shindano la mwaka huu JF itashirikiana na mshirika wake wa muda mrefu, Twaweza pamoja na wadau wengine kutoka serikalini, asasi za kiraia, mashirika yasiyo ya kiserikali na makampuni binafsi katika nyanja mbalimbali kama habari, elimu, vijana, kuimarisha ushiriki wa wananchi na utekelezaji wa maoni, wadau hawa ndio watakaoshiriki mchakato wa kupata na kuwatuza washindi,”alisema.

Melo alisema misimu iliyopita ya Shindano la ‘Stories of Change’ (SoC), takribani machapisho 6,000 yaliwasilishwa ndani ya JamiiForums.com kutoka kwa wananchi.

Melo alieleza kuwa miongoni mwa Maudhui yaliyowasilishwa, yamechangia kuboresha mifumo ya utoaji wa huduma katika Sekta ya Umma na Binafsi

Kuhusu vigezo na masharti ya kushiriki katika shindano hilo, Melo alisema mshiriki anatakiwa kutayarisha andiko linaloelezea Tanzania tuitakayo lenye maoni ya kiubunifu ambayo yanaweza kutekelezeka ndani ya miaka 5, 10, 15 hadi 25 ijayo katika nyanja mbalimbali mfano elimu, afya, teknolojia, uchumi, mazingira, miundombinu.

Melo aliendelea kutaja vigezo hivyo ikiwemo,” Aandiko liwe kwa lugha ya kiswahili au kiingereza lenye maneno kuanzia 700 hadi 1,000 matumizi ya picha , video, vielelezo vingine yanaruhusiwa ili kuongeza uzito wa wasilisho lakini pia machapisho yanatakiwa kuwa halisi na hayajawahi kuchapishwa sehemu nyingine yoyote”

Kwa Upande wa Mkurugenzi wa Uchechemuzi wa TWAWEZA, Annastazia Rugaba, alisema moja kati ya kazi zao ni kuhakikisha wananchi wanapaza sauti zao na zinatiwa maanani na Serikali kuanzia Serikali za Mtaa hadi Serikali Kuu.