January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika Ibada ya Ijumaa Kuu iliyofanyika katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Yohana-Maria Mzeyi Parokia ya Mlimani Chato mkoani Geita leo tarehe 10/04/2020.(Picha ya Maktaba)

Msimamo wa Magufuli wawakosha maaskofu

Na Waandishi Wetu, Dar mikoani

VIONGOZI wa dini wamepongezwa uamuzi Rais John Maguful wa kuruhusu
Watanzania kuendelea kufanya shughuli zao za kila licha ya kuwepo
ugonjwa wa Corona, huku akiwahimiza kuzingatie maelekezo ya Serikali
kuhusiana na namna ya kujikinga na ugonjwa huo.

Pongezi hizo kwa Rais Magufuli zimetolewa jana kwa nyakati tofauti na
viongozi hao wa dini wakati wa Ibada ya Pasaka.

Askofu David Mabushi wa Kanisa la International Evangelical Assembly
God Of Tanzania (IEAGT) katika salaam zake za Pasaka kwa waumini wa
Kanisa hilo, alisema iwapo Watanzania wangezuiwa wasitoke ndani, hali
ya watu wengi ingekuwa mbaya.

Askofu Mabushi alisema Watanzania wana kila sababu ya kutumia vyema
huruma ya Rais Magufuli kwa kuzingatia maelekezo yote yanayotolewa na
wataalam wa afya kuhusu njia mbalimbali za kujikinga na ugonjwa wa
Corona.

Alisema ugonjwa huo hivi sasa umekuwa tishio duniani kote, ambapo hata
mataifa makubwa yenye uwezo wa kifedha na utaalamu wa hali ya juu
yanahangaishwa na ugonjwa huo, hivyo kila Mtanzania anapaswa
kuzingatia suala la kunawa mikono kila wakati kwa lengo la kujikinga
na ugonjwa huo.

Alisema mataifa mengi ambayo yamezuia wananchi wake wasitoke nje yana
hali mbaya kutokana na watu kushindwa kufanya kazi, hivyo kukosa
kipato cha kuwaingizia riziki.

Alisema hali hiyo kama ingetokea Tanzania watu wengi wangepata shida.
“Watanzania tuna kila sababu ya kumpongeza Rais Magufuli wetu kwa
hekima na busara kubwa aliyotumia ya kuturuhusu kuendelea kufanya kazi
zetu za kila siku. Lakini pia kutokufunga nyumba za ibada ambapo
ameelekeza watu waendelee kuzingatia maelekezo yanayotolewa na
wataalamu wetu kuhusu kujikinga na maambukizi ya Corona,”alisema na
kuongeza;

“Kikubwa tunachoweza kukifanya mbali ya hatua za kitaalamu kuhusu
kujikinga na ugonjwa wa Corona ni kumrejea Mungu, kwani yeye ndiye
muweza wa kila jambo.

Hivyo maombi yetu kwake yanaweza kupokelewa na kuondoa ugonjwa huu,
hata enzi za mitume gharika kama hili lilitokea, lakini watu
walipomrejea Mungu maradhi yaliondoka.”

Kwa upande wake katibu wa Kanisa hilo, Leonard Kajiba aliwakumbusha
waumini wote kuwa katika kipindi hiki cha sikukuu ya Pasaka
wasiwaruhusu watoto wao kutembea ovyo mitaani, ambako wanaweza kupata
maambukizi ya Corona bila ya wao kujua.

“Niwakumbushe ndugu zangu umuhimu wa kuzingatia maelekezo yote kuhusu
kujikinga na gonjwa hili, tuchukue tahadhari sana, tusipuuze, niwaombe
kwa sikukuu hii tuwe karibu na watoto wetu, tusiwaruhusu kutembea
ovyo, na pia tuache utamaduni uliozoeleka wa kubusiana mashavuni kwa
ajili ya kutakiana kheri ya Pasaka kwani  ni hatari,” alisema Kajiba.

Kwa upande wake Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Central
Tanganyika (DCT), Dkt. Dickson Chilongani, amesema katika uchaguzi wa
mwaka 2020, ni vema Watanzania wakawachagua viongozi wacha Mungu kama
ilivyo kwa Rais John Magufuli. Hata hivyo alisema asemi hivyo kwa
ajili ya kumpigia debe.

Askofu Dkt. Chilongani alitoa kauli hiyo jana wakati akihubiri katika
ibada ya Pasaka iliyofanyika Kanisa Kuu la Roho Mtakatifu jijini
Dodoma.

Alimshukuru Rais Magufuli kwa uamuzi wake wa kutokuzuia ibada
makanisani akisema amefanya hivyo kwa sababu ni mcha Mungu.

Alitumia fursa hiyo kuwaomba Watanzania kumuombea na kumuunga mkono
Rais Magufuli. Askofu alisema kuwaruhusu waumini waendelee kukutana na
kusali kwa pamoja ni jambo jema linalopaswa kupongezwa na watu wote
kwani wanapata nafasi ya kumlilia Mungu kuhusu janga kubwa la Corona
ambalo limeikumba dunia.

Alifafanua kuwa Rais Magufuli ni kiongozi wa mfano anayepaswa kuigwa
na dunia, kwani kitendo cha kutupa nafasi  waendelee kumlilia Mungu
katika makanisa ni cha kuungwa mkono.

Aliongeza kwamba hata kule walikozuiwa kusali bado maambukizi ni
makubwa tu, hivyo ni muhimu kuendelea kufuata ushauri wa wataalamu wa
afya.

Hata hivyo alisema ulimwenguni kote watu wanaishi katika nguvu za giza
na ndiyo maana Mungu anaendelea kufanya matengenezo kila wakati, hivyo
magonjwa kama Corona na mengine hayana budi kutokea.

***Uchaguzi

Kuhusu uchaguzi mkuu, Dkt. Chilongani alisema ni wakati kwa Watanzania
kuangalia viongozi wacha Mungu wasioegemea kwa waganga wa jadi, kwani
wanaweza kulipeleka Taifa pabaya. Hata hivyo alisema hampigii kampeni
Rais Magufuli, lakini ni kiongozi mcha Mungu wa kweli anayejua
anachokifanya.

***Barakoa

Naye Kiongozi wa Kanisa la Inuka Uangaze, Mtume Boniface Mwamposa,
aliwataka Watanzania wajilinde na ugonjwa wa Corona kwa kuhakikisha
wanavaa barakoa bila aibu.

Akizungumza wakati wa ibada ya Pasaka, Mwamposa alisema hakuna sababu
ya mtu kuona aibu kuvaa Barakoa kwa ajili ya  kujikinga Corona.

“Ukimuona mtu amevaa barakoa kanisani siyo kwamba hamuamini Mungu,
isipokuwa anajikinga na Corona. Hakuna sababu ya kuona haya kuvaa
barakoa kanisani au barabarani. Ni muhumu kufuate masharti kama
Serikali inavyoelekeza,”alisema na kusisitiza;

“Usimjaribu Mungu wako kwa kusema eti umeokoka huwezi kufuata
maelekezo ya Serikali jinsi ya kujikinga na ugonjwa wa Corona, hivyo
utakufa lazima ujikinge huku ukimuomba Mungu atuepushe na ugonjwa
huu.”

Alisema makanisani waumini wanakaa mita moja kutoka kiti kimoja hadi
kingine, hivyo hivyo wanapokuwa nyumbani wanatakiwa wakae mbalimbali
wanawe mikono na kutogusana.

***Tamko la wachungaji TAG

Wakati huo huo, Wachungaji wa makanisa ya Tanzania Assemblies of God
(TAG) mkoani Tabora wameunga mkono juhudi kubwa zinazofanywa na
Serikali katika kupambana na Corona.

Pongezi hizo zimetolewa jana katika ibada ya Pasaka iliyofanyika jana
katika Kanisa la TAG-Kitete Christian Center (KCC) lililopo mjini
Tabora.

Akihubiri katika ibada hiyo Mwangalizi wa Makanisa ya TAG Tabora
Mjini, Cheyo Mwasongela alisema Rais Magufuli ni mfano wa kuigwa kwa
viongozi wa mataifa mengine hapa duniani.

Alisema kuwa maisha ya mwanadamu yako mikononi mwa Mungu, hivyo
kitendo cha Rais kutozuia ibada na kuagiza viongozi wa madhehebu yote
kumwomba Mungu ili atuepushe na ugonjwa huu kinaonesha jinsi alivyo na
hofu kubwa mbele za Mungu.

Alieleza kusema kuwa wachungaji na waumini wa makanisa ya TAG wanaunga
mkono juhudi zote zinazofanywa na Serikali na maelekezo yote
yanayotolewa watayasimamia ipasavyo ili kuhakikisha maambukizi ya
ugonjwa huo yanakoma.

Aliahidi kuwa wataendelea kumwombea Rais na wasaidizi wake ili Mungu
aendelee kuwalinda na kuwaepusha na maambukizi ya virusi vya ugonjwa
huo.

“Tutaendelea kumuunga mkono Rais wetu na kumwomba Mungu ili aendelee
kumtetea na kumwongoza katika utendaji wake, tutaendelea kumwomba
Mungu ili atuondolee janga hili la ugonjwa wa COVID-19,”alisema.

Kwa upande wake Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la TAG-Kitete  Christian
Center, Paul Meivukie alisema kuwa kifo na ufufuko na Yesu Kristo
kinaonesha jinsi Mungu alivyompenda mwanadamu na kuchukua taabu  zake
zote.

***Askofu Minde

Askofu wa Jimbo Katoliki Moshi, mkoani Kilimanjaro, Mhashamu Ludovick
Joseph Minde, ALCP/OSS, aliwataka Watanzania hasa Wakristo Jimbo
Katoliki Moshi kuwaombea wenzao walioko kwenye Mataifa ambayo
hawakupata nafasi ya kusali Ibada ya Pasaka kwenye nyumba za Ibada
moja kwa moja.

Askofu Minde alitoa rai hiyo jana wakati wa Ibada ya Misa Takatifu ya
Sikukuu ya Pasaka iliyofanyika katika Kanisa la Kristo Mfalme lililoko
Moshi.

“Kuna wenzetu maeneo mbalimbali hapa Duniani ambao wanahitaji sala na
maombi yetu kwa kuwa tumejaliwa neema ya kushiriki Ibada ya Pasaka
moja kwa moja kutoka nyumba za Ibada.

Ni Neema ya pekee tuliyojaliwa na Mwenyezi Mungu, hivyo tuitumie
kuwaombea wenzetu ambao hawakupata fursa kama hii kutokana na janga la
Corona,” alisema.

Askofu Minde aliendelea kusema kuwa sala na maombi ya Watanzania
katika Pasaka ya mwaka huu kutasaidia kujua kuwa Mungu hajawaacha na
kwamba bado yuko pamoja nao.

“Hali si nzuri kwa baadhi ya wenzetu, nimeongea na Askofu wa Jimbo Kuu
Katoliki Mombasa nchini Kenya ananiambia hali huko si nzuri hivyo
tuwaombee”.Alisema.

Aidha alirudia kauli yake ya kuwataka waumini kuendelea kufuata
maelekezo yanayotolewa na Serikali na wataalam wa afya
yatakayowawezesha kuuepuka ugonjwa wa COVID-19 unaosababishwa na
virusi vya Korona.

Askofu Minde pia aliwaasa waamini kuitumia sherehe ya Pasaka kumrudia
Mungu kwa toba wakati huo huo wakizingatia maadili mema katika nafasi
walizojaliwa ndani ya jamii ikiwemo makazini.

“Ni kweli tumemaliza kipindi cha toba, ila toba haijaisha, tuendelee
nayo ili kujenga maadili mema mingoni mwetu na hii ndiyo maana halisi
ya Pasaka”, alisema.

Imeandikwa na Suleiman Abeid,Shinyanga
Na Heckton Chuwa, Moshi na waandishi wetu, Allan Ntana, Tabora na Dodoma na Dar