April 30, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mshama:Vijana jitokezeni mzunguko wa pili wa uboreshaji wa Daftari la kudumu la wapigakura

 

Na Penina Malundo,Timesmajira

UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM),imetoa onyo  kwa watu wote wanaonuia kuwatumia ,kuwavuruga vijana kufanya vurugu,kuwadanganya vijana hao kutoshiriki katika  zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura awamu ya pili,ili wasiweze kutimiza   wajibu wao wa kikatiba.

Aidha wametoa  wito kwa vijana wote nchini kujitokeza kwa wingi kushiriki katika zoezi la uboreshaji wa Daftari  hilo ambalo, linalotarajia kuanzia Mei Mosi hadi Julai 04 Julai 2025, kama lilivyotangazwa rasmi na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam,Katibu wa Idara ya Uhamasishaji na Chipukizi Uvccm Taifa,Jessica Mshama wakati akiongea na waandishi wa habari amesema wanatoa onyo kali la kuacha mara moja tabia hiyo kwani Tanzania ni nchi inayofuata misingi ya sheria na katiba, na kila kijana ana haki ya msingi ya kushiriki katika taratibu za kidemokrasia kwa amani, uhuru na utulivu.

“Kujitokeza kwa wingi na kushiriki zoezi hili kwa uzalendo na uwajibikaji wa hali ya juu, UVCCM tunawaasa vijana wote na wananchi kwa ujumla,msidanganywe na watu wasio na mapenzi mema na Taifa letu, wanaopotosha dhamira njema ya uboreshaji wa daftari.

“Ni muhimu kila mmoja wetu kujitokeza na kutimiza wajibu huu wa kizalendo na Kidemokrasia kwa mustakabali bora wa taifa letu. Tanzania imara, maendeleo endelevu, yanaanza kwa kila mmoja wetu kushiriki kikamilifu katika mchakato huu wa kitaifa,” amesema.

Ametoa wito kwa vijana wa Kitanzania  kuwa wazalendo wa kweli na kulitumikia taifa lao kwa upendo na kuhakikisha wanalinda na kudumisha amani, ambayo ndiyo msingi wa maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kisiasa.

Amesema amani ndiyo nguzo inayowawezesha kuendelea mbele, na vijana wanayo nafasi ya kipekee ya kuilinda kwa nguvu zote.”Ndio maana  UVCCM tunawahimiza vijana kumuunga mkono kwa vitendo Rais  Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye anaendelea kuthibitisha mapenzi makubwa kwa vijana wa taifa hili.

“Katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wake kuanzia Novemba 2020 hadi Februari 2025, ajira zaidi ya milioni 8 (8,084,204) zimezalishwa, sawa na utekelezaji wa asilimia 115 ya lengo la kutengeneza ajira milioni 7 katika sekta ya umma na binafsi,”amesema Mshama.

Amesema  ajira hizo zimezalishwa kupitia miradi ya kimkakati kama ujenzi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP),Reli ya Kisasa ya SGR,Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere,Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato,pamoja na fursa za ajira katika sekta za elimu na afya.

Wakati huo huo akizungumzia ziara ya Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana Chama cha  Mapinduzi(UVCCM),Mohammed Ali Kawaida  amesema ameendelea kuimarisha uhai wa UVCCM na kusukuma mbele ajenda ya maendeleo ya vijana nchini.

Amesema Kawaida ameendelea na ziara yake maalum kuanzia Aprili  25, 2025 ambapo ilianza katika Mkoa wa Njombe ambapo Mwenyekiti alikutana na vijana na wanachama wa UVCCM, akisisitiza umuhimu wa mshikamano, uzalendo, na ujenzi wa uchumi wa vijana.