Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma
SERIKALI kupitia Bohari ya Dawa(MSD) inatekeleza mpango maalumu wa kuongeza upatikanaji wa huduma za uchujaji wa damu ikiwa ni sehemu ya matibabu ya figo, hivyo kupunguza gharama za huduma hiyo.
Hayo yamesemwa jijini hapo leo Machi 19,2025 na Mkurugenzi Mkuu wa MSD,Mavere Tukai wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa Bohari ya Dawa katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita.
Tukai amesema kutokana na uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali ya
awamu ya sita, hadi kufikia mwezi Februari 2025, idadi ya mashine imeongezeka na kufikia mashine 137 kutoka mashine 60 na hivyo kuongeza idadi ya hospitali zilizopokea mashine kutoka Bohari ya Dawa kutoka hospitali sita zilizokuwepo mwaka wa fedha
2021/22 na kufikia hospitali 15 mwaka 2024/25.
“Uwekezaji huu uliofanyika umegharimu
kiasi cha shilingi bilioni 7.7.
Katika hospitali hizi, hospitali 11 zimeanza kutoa huduma na hospitali nne zipo katika hatua ya matengenezo,”amesema Tukai.
Tukai ametaja baadhi ya hospitali zinazotoa huduma ni pamoja na Hospitali za Rufaa za Mikoa ya Amana, Mwananyamala ,Temeke, Morogoro, Katavi, Tumbi, Chato, Sekoe Toure na UDOM Hospitali.
“Mkakati huu wa usambazaji wa mashine za dialysis unalenga kupunguza gharama
ambapo kwa sasa gharama zinazotozwa ni kati ya shilingi 200,000 na shilingi 230,000 na matarajio ni kuweza kupunguza na kuwa chini ya shilingi 100,000 kwa ‘session’moja.
Vilevile Tukai ameeleza kuwa maboresho yanayoendelea na uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali, mapato ya MSD yameendelea kuongezeka kutoka shilingi bilioni 315.1 kwa mwaka wa fedha 2021/22, hadi kufikia shilingi bilioni 553.1 kwa mwaka wa fedha 2023/24 ikiwa ni ongezeko la shilingi bilioni 238 ambayo ni sawa na asilimia 76.
Amesema katika kipindi cha Julai 2024 hadi Februari 2025 imepata mapato ya thamani ya shilingi bilioni 400.2 sawa na asilimia 115 ya lengo la kusambaza bidhaa za afya zenye thamani ya shilingi bilioni 346.6.
“Kutokana na kuimarika kwa utendaji wa Bohari ya Dawa, makusanyo ya fedha kutoka kwenye vituo vya kutolea huduma za afya yameendelea kuongezeka katika kipindi cha Serikali ya awamu ya sita ambapo makusanyo yameongezeka kutoka shilingi bilioni 54.2 mwaka 2021/2022 hadi kufikia shilingi bilioni 118.9 mwaka 2023/2024,” amesema Tukai.
Pamoja na hayo Tukai amesema Serikali kupitia Bohari ya Dawa inatarajia kutekeleza mradi wa kuhifadhi mazingira kwa kutumia umeme wa jua “Green Project”
“Mradi huu kwa ujumla unatarajiwa kugharimu
kiasi cha shilingi bilioni 36.6 na kiasi cha shilingi bilioni 13.8 kinatarajia kutolewa kwa
ajili ya usimikaji wa nishati itokanayo na jua kwenye mikoa ya Dodoma, Dar es Salaam,Tanga ,Mtwara na Mwanza.
” Uwepo wa nishati hii itasaidia kuendana na mpango mzima wa Serikali wa kuhimiza matumizi ya nishati mbadala na utunzaji wa mazingira,
utasaidia kuimarisha uhifadhi wa bidhaa za afya na kuokoa fedha nyingi zinazotumika
katika shughuli za kila siku za Bohari ya Dawa,”amesema Tukai.


More Stories
NACTVET yawahakikishia wadau, usimamizi thabiti wa ubora wa elimu ya Ufundi na Amali
Wasira awataka Wenyeviti CCM kuiga mfano Mkoa wa Mbeya
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali,yajizatiti kuboresha uwezo wa Mawakili wa Serikali