November 19, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

MSD yaanika mikakati kwa mwaka 2023/2024

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira,Online Dodoma

BOHARI ya Dawa (MSD) imeanika mikakati yake kwa mwaka wa fedha 2023/24, huku imesema utekelezaji wa majukumu yake unaenda sambasamba na utekelezaji wa maelekezo ya maboresho ya utendaji yaliyotolewa Machi, 2022 na Rais Samia Suluhu Hassan.

Hayo yamesemwa mwishoni mwa wiki jijini Dodoma na Meneja Mipango, Ufutiliaji na Tathmini wa MSD, Hassan Ibrahim, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa shughuli na mafanikio ya MSD.

Hivyo, Ibrahim amesema Bohari ya Dawa inapitia mifumo yote ya utendaji na uendeshaji ikiwamo maboresho ya mnyororo wa ugavi, usimamizi wa utendaji na mifumo ya TEHAMA ili kuendana na kasi ya ongezeko la ujenzi wa vituo vya kutolea huduma za afya vinavyojengwa na Serikali chini ya uongozi wa Rais Samia.

Hatua hiyo ya MSD inalenga kuhakikisha malengo ya Serikali katika upatikanaji wa bidhaa za afya yanafikiwa.

Kwa mujibu wa Ibrahim, mikakati ya MSD kwa mwaka wa huu wa fedha wa 2023/24 ni kuimarisha upatikanaji wa bidhaa za afya kwa uboresho matumizi ya takwimu za maoteo, kuhakikisha bidhaa zote za afya zinakuwa na mikataba ya muda mrefu na kuimarisha ushirikiano na wazalishaji wa ndani kwa kutoa fursa kwa wazalishaji wa ndani na kununua kutoka kwa wazalishaji wa nje pale inapobidi.

Malengo mengine kwa mujibu wa Ibrahim ni kuanza uzalishaji wa mipira ya mikono kwa Kiwanda kilichopo kijiji cha Idofi, mkoa wa Njombe, ambacho kitaokoa fedha za kigeni sh. bilioni 33 kwa mwaka.Kiwanda hicho kinatarajia kuanza uzalishaji Septemba, mwaka huu.

Mikakati mingine ni kufanya ugatuzi wa majukumu yaliyokuwepo makao makuu na kuyapeleka katika Kanda ili kuboresha utendaji.

Aidha, anataja mikakati mingine kuwa ni kuanza kutekeleza miradi ya uanzishaji wa viwanda vya bidhaa za afya eneo la Zegereni, mkoa wa Pwani na uanzishaji wa viwanda vya Pamba tiba.

Mkakati mwingine ni wa ujenzi wa maghala ya kisasa katika mikoa ya Dodoma, Mtwara na Kagera kwa lengo la kuongeza nafasi za kuhifadhi bidhaa na kuimarisha ubora wa bidhaa za afya.