November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

MSD na mikakati ya uzalishaji bidhaa za afya, vifaa tiba

Na Reuben Kagaruki,TimesMajira,Online, Dodoma

KWA mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi iliyofanyika mwaka jana (2022) Tanzania ina watu milioni 61.7. Lengo la kufanyika kwa Sensa hiyo, pamoja na mambo mengine ni kuiwezesha Serikali kujua idadi ya watu wake ili kuweza kupanga mipango ya kuwahudumia wananchi wake.

Kutokana na idadi ya Watanzania kuongezeka, Serikali imezidi kupanga mipango mbalimbali kwa ajili ya kuhakikisha wanapata huduma bora zikiwemo za afya.

Mfano, Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan inakusudia kujenga zahanati kila kijiji nchi nzima ili kusongeza huduma za afya jirani na wananchi.

Aidha, katika maeneo mbalimbali ya nchi, Watanzania wanashuhudia kasi ya ujenzi wa vituo vya afya na hospitali kila wilaya. Ili zanahati hizo ambazo Serikali inajenga kila kijiji, pamoja vituo vya afya na hospitali za wilaya ziweze kufanyakazi na kutoa huduma bora kwa Watanzania ni lazima ziwe na bidhaa za afya pamoja na vifaa tiba.

Mbali na Serikali kujenga vituo vipya vya kutolea huduma, tunashuhudia ikiendelea kupandisha hadhi vituo vya afya ili kuweza kupanua huduma za afya nchini.

Maendeleo hayo yanapotokea Bohari ya Dawa (MSD) inakuwa na jukumu kubwa la kuhakikisha vituo vyote vya kutolea huduma za afya nchi vinawezeshwa kupata bidhaa za afya ikiwa ni pamoja na vifaa tiba, mashine mbalimbali na dawa.

Kwa hiyo kujengwa vituo vipya vya afya na vingine kupandishwa adhi, kunawafanya watanzania kuelekeza macho yao kwa MSD, ambayo ni taasisi inayohusika na kununua, kuhifadhi na kusambaza bidhaa afya kwa kwa vituo vya umma vya kutolea huduma za afya nchini.

Ndiyo maana mara kadhaa tumekuwa tukisikia malalamiko kadhaa yahusuyo bidhaa za afya, aidha ni kukosekana au kuchelewa,

MSD kwa kutambua dhamana kubwa iliyonayo kwa Watanzania ya kuhakikisha wanapata vifaa vya afya na vifaa tiba hivi karibuni iliandaa semina ya wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari iliyofanyika mkoani Dodoma na kuanika mikakati mbalimbali inayochukuliwa na taasisi hiyo, ili kuhakikisha dhamira ya Serikali kujenga ya kujenga vituo vya afya na upandishaji hadhi vituo vingine inaenda sambamba na upatikanaji wa bidhaa za afya pamoja na vifaa tiba.

, kwanini shida hii? Je, ni tatizo la MSD? ambayo inakiri kupokea fedha za kununulia bidhaa za afya kwa wakati ama kuna mambo mengine ambayo tunapaswa kuyafahamu? Basi katika siku mbili hizi lazima tufahamu vizuri masuala mazima ya mnyororo wa ugavi wa bidhaa za afya.

Kwa sasa MSD ambayo imeanzishwa mwaka 1993 kwa Sheria ya Bunge No. 13 na iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2021 na kuongeza uzalishaji wa bidhaa za afya, itatumia Kampuni Tanzu kusimamia uendeshaji wa shughuli zake za uzalishaji wa bidhaa za afya.

Akitoa mada kwenye semina hiyo ya wahariri wa vyombo vya habari, Kaimu Meneja Mipango, Tathmini na Ufuatiliaji wa MSD, Hassan Ibrahim, amesema, sababu za kuanzisha Kampuni Tanzu kuondoa urasimu na kuendana na mabadiliko ya uendeshaji wa viwanda.

Aidha, anataja sababu nyingine kuwa ni fursa ya kuingia ubia (joint venture) na wawekezaji wengine.

“Kujiendesha kibiashara na kuweza kutoa huduma stahiki kwa jamii na
kuongeza wigo wa uzalishaji na kuruhusu MSD kujikita kwenye ununuzi, utunzaji na usambazaji wa bidhaa za afya,” anasema na kutaja sababu nyingine kuwa ni kuwa na chama inayojitambua.

Kwa mujibu wa Ibrahim, sababu nyingine ya kuanzisha kampuni Tanzu ni kuongezeka uwajibikaji kwa njia ya “limited company” na kutengeneza mfumo imara wa kiutawala kati ya kampuni mama na Tanzu

Akizungumzia kuhusu viwanda vinavyomilikiwa na MSD, Ibrahim anasema ni pamoja na Kiwanda cha Barakoa (Surgical Mask) amvacho kimekamilika na kinafanya kazi.

Anafafanua kwamba kiwanda hicho kimezalisha barakoa zaidi ya milioni 5.8.

Kiwanda kingine, ni kiwanda cha Barakoa – N95, ambacho anasema kimekamilika na kipo katika hatua za kupata idhini ya ubora wa bidhaa zake.

Kingine ni kiwanda cha Mipira ya Mikono – Gloves, ambacho kipo katika hatua mbalimbali za kukamilika ambapo kimefikia asilimia 70.

Akizungumzia kiwanda cha Barakoa, Ibrahim anasema kilianza kazi rasmi Agosti 2020. Anaeleza kwamba uanzishaji wa kiwanda ulilenga kukabiliana na janga la uviko-19 kwa wakati huo.

***Mafanikio

Kuhusu mafanikio, anasema kiwanda kiliwezesha bei ya barakoa kupungua kutoka sh. 1,600 hadi kufikia sh.500, hadi sasa barakoa milioni 5.8 zimezalishwa.

Kuanzishwa kwa kiwanda hicho kumewezesha MSD kuacha kuagiza barakoa kutoka nje ya nchi, na kutegemea zinazozalishwa ndani. ” Kwa uamuzi huu MSD imeokoa fedha za kigeni na kuhakikisha ubora wa barakoa husika,” anasema Ibrahim.

Anaongeza kuwa barakoa hizi hutumika kumkinga mtoa huduma na anayepatiwa huduma kwenye vituo vya afya

***Uwezo wa Kiwanda cha Barakoa

Akieleza uwezo wa kiwanda, Ibrahim anasema ni kuzalisha barakoa 80 kwa dakika.

Kwa upande wa gharama za kiwanda, anasema mradi huu umegharimu sh. bilioni 1.4 hadi kukamilika

***Kiwanda cha Barakoa – N95

Ibrahim anasema kiwanda kimezinduliwa Machi 2023.

***Matarajio

Akielezea matarajio ya MSD, Ibrahim anasema ni kuacha kuagiza barakoa kutoka nje ya nchi, na kutegemea zinazozalishwa ndani, hivyo kuokoa fedha za kigeni na kuhakikisha ubora wa barakoa husika.

“Barakoa hizi humkinga mtumiaji dhidi ya vimelea na vijidudu.
Barakoa hizi hutumika katika maabara za magonjwa mbalimbali na maeneo ya hospitali, viwandani na migodini kutokana na uwezo wake wa kuchuja,” anasema.

***Upatikanaji wa Kiwanda

Ibrahim, anasema kiwanda kimepatikana kutoka kwa wadau wa maendeleo kupitia UNIDO.

***Uwezo wa Uzalishaji

Anasema kiwanda kina uwezo wa kuzalishaji barakoa 100 – 150 kwa dakika

****Kiwanda cha Mipira ya Mikono

Kuhusu kiwanda hicho, Ibrahim kiwanda kinatarajia kuanza uzalishaji mwezi Julai 2023.

***Matarajio

Akizungumzia matarajio, Ibrahim anasema ni kukidhi asilimia 83.4 ya mahitaji ya gloves nchini. “Sasa kinatoa ajira 136 na kikianza kazi kitatoa ajira zaidi ya 200 za moja kwa moja na zile zisizo za moja kwa moja.

Kuokoa fedha za kigeni na kuhakikisha ubora wa barakoa husika
Kitatumia malighafi za nchini kutoka Muheza (Tanga) na Ifakara (Morogoro),” anasema Ibrahim.
 
Kuhusu uwezo wa kuzalisha, Ibrahim anasema kina uwezo wa kuzalisha gloves 10,000 kwa saa, sawa na jozi 86,400,000 kwa mwaka.

Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Mavere Tukai anasema kabla ya kufikia hatua ya kujenga viwanda na kufungua kampuni tanzu, ulifanyika upembuzi yakinifu ili kujiridhisha tija ya uanzishwaji wake.

Anasema walibaini ipo tija ya kufanya hivyo. “Tunaamini kampuni tanzu itatusaidia kama walivyotangulia kuzungumza wenzangu, lakini pia hatutaishia hapo, tutajenga viwanda vingi zaidi ikiwemo vya dawa, tunafanya tathmini pia ya kuwa na kampuni ya uzalishaji Oxygen za hospitali na maeneo mengine yenye uhitaji,” anasema Tukai.

“Hatulengi tu kupunguza gharama za kununua kutoka nje kwa sababu inaweza isipungue sana kwa kuanzia, lakini tutakuwa na uhakika wa uzalishjai na
ikiwezekana kuuza nchi jirani,” anasema.

Naye Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile alisema suala hili lilikuwa likisubirtiwa kwa muda mrefu na wananchi, tena huenda limechelewa kufanyiwa kazi.

“Tulikuwa tukishangaa sana kuona Tanzania tuna rasilimali
nyingi hasa misitu, tungeweza hata kuanzisha mabustani ya Botanic, tunaweza kuzalisha dawa wenyewe.

Hatuna sababu ya kuedelea kuagiza kutoka nje, naamini tutafanikiwa,” anasema Balile.

MSD wapo katika kipindi muhimu ya mabadiliko kwa lengo la kuongeza tija kwenye uzalishaji, ununuzi, uhifadhi, usambazaji wa dawa kwa wananchi
ili ziwafikie zikiwa salama.