Na Raphael Okello, Timesmajira Online,Musoma
MKUU wa Mkoa wa Mara, Kanali Evance Mtambi ameipongeza Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mara(MRPC) kuanzisha tuzo kwa waandishi wa habari mkoani humo watakaoandika habari zenye kuleta matokeo bora kwa jamii.
Kanali Mtambi amesema hayo leo wakati akifungua mdahalo wa “Mara bora kwa uwekezaji na kuishi” ulioandaliwa na MRPC kwa kushirikisha na wadau wa maendeleo mkoani humo.
Amesema mpango huo wa kuanzisha tuzo utawafanya waandishi wa habari ndani ya Mkoa huo kuongemza juhudi za uandishi bora katika kutangaza rasilimali zilizopo Mara.
Ametaja baadhi ya rasilimali na vivutio ndani ya Mkoa huo ni pamoja na makumbusho ya Baba wa Taifa,Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere,Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na mapori ya akiba ya Grumet na Ikorongo.
Vivutio vingine ni Ziwa Victoria, madini, kilimo na mifugo na kwamba vikitangazwa vyema Mkoa wa Mara utakuwa sehemu salama kwa uwekezaji na kuishi.
“Niwaombe waandishi wa habari mkoani hapa, wadau wa maendeleo na watendaji wa serikali kuhakikisha kuwa mnatangaza vyema fursa za uwekezaji kwa wananchi ndani ya Mkoa na duniani kwa ujumla,”amesema.
Mwenyekiti wa MRPC, Mugini Jacob amesema lengo la mdahalo huo ni kujadili na kuona namna gani waandishi wa habari wanaweza kuchangia katika kutangaza fursa za uwekezaji na mazingira bora ya kuishi.
Mugini amesema katika kuhakikisha kuwa fursa za uwekezaji zinatangazwa, klabu hiyo imeanzisha tuzo kwa waandishi wa habari mkoani humo watakaotangaza na kuandika habari bora katika vyombo mbalimbali vya habari.
Ametaja habari hizo zitakazoanza kutolewa tuzo ndani ya mwaka huu ni zile zitakazohusu madini, utalii, uhifadhi, kilimo, mifugo, biashara, ukatili wa kijinsia na uvuvi.
Baadhi ya wadau wa maendeleo wakichangia hoja katika mdahalo huo waliwataka waandishi wa habari kuwasaidia katika kutangaza shughuli za uwekezaji na fursa mbalimbali na kuepusha taarifa zinazoweza kuwafukuza wawekezaji.
More Stories
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa Â
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi